Gachagua ataka Wakenya kukumbatia mabadiliko katika baraza la mawaziri
NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa Wakenya kudumisha umoja na kukumbatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyotangaza Rais William Ruto akiyataja kama ushindi kwa taifa.
Alisema kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri, kutaongeza ufanisi huku akiwakemea wale wanaojaribu kuwagawanya Wakenya.
“Nimeona watu wengi na kila aina ya uchambuzi kuhusu nani alishinda na nani alipoteza lakini jambo zima ni ushindi kwa watu wa Kenya,” alisema jana katika kijiji cha Ntukuruma, Nanyuki, Kaunti ya Laikipia katika mazishi ya Bi Susan Muthoni Kiiru Wanjohi mamake Katibu wa Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau, ambapo pia alisoma rambirambi za Rais William Ruto kwa familia.
Wakati huo huo, Naibu Rais alilaani uharibifu wa mali na machafuko yaliyotokea wakati wa maandamano ya amani ya hivi majuzi.
“Sote tuendelee kuwa pamoja kama nchi, tumepitia kipindi kigumu.
Waliotumia maandamano ya amani yenye nia njema kupora mali, kuiba na kulemaza ni wajinga,” alisema.
Bw Gachagua, aidha, alikashifu waliotumia fursa hiyo kubuni propaganda za kuwapotosha Wakenya akisema kuwa Wakenya ni watu wenye akili.
“Kuna wajinga zaidi ambao walijaribu kutumia fursa ya hali ili kusuluhisha tofauti za kisiasa. Wakenya wana akili sana; wanaona kutoka mbali, wanachanganua na wanaelewa,” akasema.