Familia yalilia haki mwili wa mwanao aliyefuzu NYS ukipatikana mochari
FAMILIA moja katika Kaunti ya Kirinyaga inalilia haki baada ya mwili wa mwanao ambaye alifuzu juzi kutoka kwa Idara ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kupatikana kwenye mochari.
Mwili wa marehemu James Macharia, 26, ambaye alitoweka Jumamosi ya Julai 21 ulikuwa na majeraha sehemu mbalimbali. Pikipiki ambayo alikuwa akitumia kabla ya mauti yake na ilikuwa ya jirani yake, bado haijapatikana.
Baada ya kumtafuta kwa zaidi ya wiki moja, familia hiyo ilipata mwili wake kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kerugoya.
“Tulimsaka mwana wetu katika maeneo mbalimbali baada ya kukosa kuja nyumbani kijijini kwetu Karira lakini tukaishia kupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti,” akasema Simon Wanjohi, mjomba wa marehemu.
Kwa mujibu wa mamake Rose Waitherera, mwanawe alitoka nyumbani kwao mji wa Ngurubani siku hiyo asubuhi na akaingiwa na wasiwasi aliposhindwa kurudi nyumbani.
“Nilipouliza, niliambiwa mwanangu alikuwa kwenye baa alipopokea simu kutoka kwa watu wasiojulikana na akaenda kukutana nao. Baadaye tulipata mwili wake kwenye mochari,” akasema Bi Waitherera.
Familia hiyo sasa inadai mwanao aliuawa na kuibiwa pikipiki na sasa wanataka haki itendeke.
“Tunataka wale ambao walimuua mwanangu wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria,” akasema Teresa Wanjiru ambaye ni shangaziye marehemu.
Aidha familia hiyo ilifichua kuwa waligundua mwanao alipigwa na kuachwa akiwa mahututi na ni wasamaria wema ndio walimpeleka katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kimbimbi kwa matibabu.
Hali yake ilibadilika na kuwa mbaya hadi akahamishwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya ambapo aliaga punde tu baada ya kufikishwa na mwili wake ukapelekwa mochari.
Tafsiri na Cecil Odongo