Habari za Kitaifa

Ruto ateua Oduor kumrithi Muturi kutokana na ‘ukwasi, ujuzi na weledi’ wa kisheria


RAIS William Ruto amemteua wakili Dorcus Agik Oduor kuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwanamke.

Rais Ruto alimteua Bi Oduor, mwenye tajriba ya juu na mweledi katika masuala ya sheria na uendelezaji wa kesi za umma kutwaa wadhifa huo ulioachwa wazi baada ya kutimuliwa kazini kwa aliyekuwa AG Justin Muturi alipovunja baraza lote nzima la mawaziri.

Jina la Bi Oduor limepelekwa katika bunge la kitaifa kupigwa msasa pamoja na mawaziri wengine aliowateua hivi majuzi katika zoezi litakaloanza Agosti 1, 2024.

Katika taarifa kwa wanahabari kutoka kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Rais Ruto alisema alimteua Bi Oduor kutokana na “ukwasi, ujuzi na weledi wake katika sheria” aliosema unatakiwa katika utekelezaji wa majukumu ya AG.

Bi Oduor ambaye amehudumu katika sekta ya umma kama wakili wa serikali kwa miaka 30 amepata umaarufu kama kiongozi wa mashtaka katika kesi mbali mbali za uhalifu.

“Nimemteua Bi Oduor kutwaa wadhifa wa mwanasheria mkuu ulio wazi, kutokana umahiri, weledi na kujitolea kwake kustawisha sheria nchini,” Rais Ruto alisema katika taarifa kwa wanahabari.

Bi Oduor, Rais Ruto alisema, amekuwa katika mstari wa mbele kustawisha sekta ya sheria kwa kuongoza na kushiriki katika kamati mbali mbali za kuangazia dosari na mapungufu ya sheria katika masuala kama vile changamoto za kiakili.

Bi Oduor aliyewahi kuteuliwa kuwa naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amehudumu kwa miaka 30 katika afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma.

Bi Oduor aliapishwa kuwa wakili wa Mahakama kuu 1992 baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha Nairobi alipofuzu katika taaluma ya uanasheria baada ya kuhitimu 1990.

Bi Oduor, anayetoka eneo la uwakilishi bungeni la Nyando anajulikana kwa ukakamavu wake katika utenda kazi katika Mahakama nchini.

Kabla ya uteuzi kuwa AG, Bi Oduor alikuwa Katibu katika masuala ya uendelezaji wa kesi za umma afisi ya DPP.

Bi Oduor, OGW, EBS, SC, Kamishna katika kamati ya sheria (KLRC) yuko na digirii ya uzamili masuala ya usimamizi wa hali tata.

Bi Oduor aliwahi kuhudumu kama naibu wa mkurugenzi wa kesi za umma (ODPP) Bw Keriako Tobiko alipokuwa DPP na pia alikuwa naibu wa Jaji Mkuu (CJ) Bernard Chunga alipokuwa DPP.

Pia amehudumu katika asasi mbali mbali na pia tume ya makabiliano ya masuala ya ardhi ya- Jaji (marehemu) Akilano Akiwumi, tume ya huduma za polisi (Ransely Commission) bodi ya kamati ya kutathmini masuala ya changamoto za akili, tume ya uchunguzi wa Kashfa ya Golden almarufu (tume ya Jaji (mstaafu) Samuel Bosire ya 2003, tume ya Kiruki ya kuwachunguza Artur Brothers almaarufu Mamuluki.

Bi Oduor atakuwa wa msaada mkuu kutokana ujuzi na uzoevu wa kazi katika sekta ya sheria.

Mbali na Bi Oduor Rais Ruto pia alimteua Bi Beatrice Asukui Moe kuwa Waziri wa Masuala ya Jumuia ya Afrika Mashariki.

[email protected]