Michezo

Malkia Strikers warambwa tena na Poland voliboli ya Olimpiki

Na JOHN KIMWERE August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

TIMU ya voliboli ya wanawake almaarufu Malkia Strikers bado inaendelea kuteleza kwenye Michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini Paris, Ufaransa baada ya kupokezwa kichapo kingine katika mechi za Kundi B.

Juhudi za warembo hao wa makocha, Japheth Munala na James Barasa kuandikisha historia ya kusajili angalau hata ushindi wa seti moja kwenye kipute hicho ziligonga ukuta usiku wa kuamkia jana walipozabwa seti 3-0 na Poland kwenye mechi yao ya pili.

Kina dada hao chini ya nahodha Trizah Atuka walikubali kichapo cha 25-14, 25-17, 25-15, baada ya hapo awali kushindwa seti 3-0 na Brazil katika mechi ya utangulizi.

Katika mechi hizo mbili walishindwa kwa muda sawa kwani Brazil ilitumia dakika 56 kuzima Malkia Strikers huku Poland ikitumia dakika 58 pekee kumaliza mchezo wao.

 

Malkia Strikers walianza michuano ya Olimpiki kwa kuchuana na Brazil ambapo pia walishindwa. Picha|Reuters

Matokeo hayo yanaashiria kuwa bado Malkia Strikers haina uwezo wa kung’ata wapinzani wao katika viwango vya dunia.

Kwenye mechi hizo mbili Sharon Chepchumba hakupewa nafasi licha ya kutarajiwa kuwa yeye ni kati ya wachezaji wawili wa kimataifa wanaotazamiwa kusaidia kikosi hicho.

”Bado tuna mechi moja dhidi ya Japan tunakolenga kujituma kisabuni kwenye juhudi zetu za kusaka angalau ushindi wa seti moja,” alisema nahodha wa kikosi hicho, Atuka.

Kenya imepangwa katika Kundi B linaloshirikisha Brazil, Japan na Poland. Nalo Kundi A linajumuisha: Ufaransa, Serbia, Marekani na Uchina. Uholanzi, Uturuki, Italia na Jamhuri ya Dominika zimepangwa katika Kundi C.

Kwenye makala ya mwaka 2020 jijini Tokyo, Japan Malkia Strikers walishindwa kufana na kumaliza katika nafasi ya 12.