Jubilee ijifunze kutokana na ODM – Murkomen
Na WYCLIFFE MUIA
SENETA wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen sasa anataka chama chake cha Jubilee kuiga mfumo wa usimamizi wa chama cha ODM na kusema anatamani sana iwapo Jubilee ingekuwa na mfumo wa uongozi kama chama hicho cha upinzani.
Akihojiwa katika televisheni moja ya humu nchini jana asubuhi, Bw Murkomen alisema chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kina nidhamu zaidi kuliko Jubilee.
“Ninatamani sana uongozi wa ODM licha ya changamoto nyingi chama hicho kinapitia,”alisema Bw Murkomen.
Bw Murkomen ambaye pia ni kiongozi wa walio wengi katika Seneti alisifu jinsi chama cha ODM kilivyodhibiti mawimbi ya kisiasa yaliyoibuka baada ya Bw Odinga kuanza kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.
“Hata wakati wa handisheki, Waziri huyo Mkuu wa zamani aliwaita wanachama wake na kuwaelezea walichozungumzia na Rais Kenyatta,”alisema Bw Murkomen akiashiria makosa ya Rais Kenyatta kushindwa kuelezea wanachama wa Jubilee makubaliano yake na Bw Odinga.
Alisema kuna haja ya Jubilee kuiga miundo ya uongozi ya ODM ili kulainisha mizozo na kuweka mfumo mwema wa kufanya maamuzi muhimu ya chama.
“ODM imedumu kwa miaka 10 na sisi tumehudumu tu kwa miaka mitano. Kuna haja ya kujifunza mengi kutoka kwa ODM,”akasema.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe kujiuzulu na kusisitiza kuwa Naibu Rais William Ruto hafai kuwania urais 2022.
Msimamo wa Bw Murathe umezua joto jingi katika Jubilee huku baadhi ya wabunge wakimtaka Rais Kenyatta kujitokeza na kueleza wazi msimamo wake kuhusu mzozo ndani ya chama chake.
Bw Murkomen alisema uongozi wa Jubilee unapaswa kuleta maridhiano ili kuzuia chama kuporomoka.
“Murathe bado ni mwanachama wa Jubilee na tunamhitaji chamani. Kuna haja ya kuwepo na maridhiano ili kuzima migawanyiko zaidi,” alisema Semeta huyo.
Naye Seneta maalum wa Jubilee Isaac Mwaura alisema ni wazi chama hicho kinaendelea kuporomoka na kumlaumu Bw Odinga kwa masaibu hayo.
“Ukweli mchungu ni kuwa ndoa ya Jubilee imefika mwisho. Raila alifanikiwa kuvunja NASA na sasa baada ya kujiunga na Jubilee, matokeo ni yale yale,”alisema Bw Mwaura.
Mbunge wa Sirisia John Waluke aliunga mkono kauli ya Bw Mwaura akisema muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga umekuwa laana kwa chama cha Jubilee.
“Kazi haijakuwa ikifanyiki tangu Raila aungane na Rais Kenyatta…Rais hashughulikii chama cha Jubilee tena. Tunataka tumsaidie Rais aondoke katika hii nyororo ambayo amewekwa na Raila,” alisema Bw Waluke.