Habari za Kaunti

Matumaini ya kurejeshwa kwa feri Mtongwe yadidimia wakazi wakiteseka

Na ANTHONY KITIMO August 3rd, 2024 2 min read

WAKAZI wa Mtongwe katika Kaunti ya Mombasa wataendelea kusafiri takriban kilomita 10 au hata zaidi ili kupata huduma za kuvuka kutoka Kisiwani Mombasa, baada ya kubainika kuwa hakuna matumaini ya kurejesha huduma za kivuko cha feri eneo la Mtongwe.

Kwa sasa wakazi hao watazidi kusongamana katika feri eneo la Likoni ambayo huhudumia takriban watu 300,000 baada ya serikali kufeli kurekebisha sehemu za kuegeshea feri. Haya yanajiri kukikosekana imani ya mradi huo kutengewa fedha zozote na serikali kuu.

Mnamo Oktoba 15, 2021, Huduma za Feri Nchini (KFS) ilisimamisha huduma za feri Mtongwe ikihoji kuwa kulikuwa na masuala ya kiusalama baada ya sehemu ya eneo la kuegeshea kusombwa na mawimbi ya baharini. Tangu wakati huo, wakazi wamekuwa wakilazimika kutembea mwendo mrefu kuvuka feri eneo la Likoni. Isitoshe, kusitishwa kwa huduma hizo kumewaacha wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wakitegemea biashara katika eneo hilo katika njia panda. Wateja waliokuwa wakinunua bidhaa katika sehemu hiyo walilazimika kubadilisha njia. Mnamo Mei 2022, Kamati ya Bunge ya Uchukuzi, kazi za umma na nyumba iliahidi kuwa huduma za feri zingerejea kabla ya mwaka kukamilika. Ahadi hizo hazikutimia licha ya Mamlaka ya Bandari Humu nchini (KPA) kutenga fedha za kurekebisha maeneo ya kuegeshea feri katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Mamlaka hiyo ilieleza kuwa kuchelewa huko kulitokana na masuala ya kikandarasi kati ya KPA na mwanakandarasi ila ikasema hilo lilishughulikiwa. Taarifa zinaeleza kuwa misingi ya maeneo hayo ya kuegeshea feri ilikuwa imeharibika kiasi cha sehemu moja kujitenga na eneo zima, ishara kuwa ingeng’oka baada ya muda.

Juhudi za wakazi kuelezea Rais William Ruto kuhusu masaibu yao alipozuru ukanda wa Pwani wiki kadhaa zilizopita hazikuzaa matunda, rais akieleza kuwa kulikuwa na mipango ya kutafuta suluhu ya kudumu.

“Tuanelewa masaibu ya wakazi wa Likoni tangu kufungwa kwa daraja la kuelea la Liwatoni ambalo lilikuwa likisababisha msongamano wa meli katika bandari. Nimezielekeza Mamlaka ya kusimamia barabara nchini (KENHA) na KPA kutafuta suluhu katika eneo la feri,” akasema Bw Ruto.

Wakazi wa Mtongwe walikuwa wakitumia daraja hilo la Liwatoni kama njia mbadala ya kivukio cha feri kabla ya serikali kulifunga kwa kuhitilafiana na njia ya meli zinazoingia na kutoka katika Bandari ya Mombasa.