Habari za Kitaifa

Ningekuwa mlanguzi wa mihadarati nisingesazwa na serikali zilizopita – Joho

Na CHARLES WASONGA August 4th, 2024 1 min read

WAZIRI mteule wa Uchumi wa Baharini na Uchimbaji Madini Hassan Ali Joho amekana madai kuwa anahusika katika ulanguzi wa mihadarati.

Bw Joho alisema hakuna ushahidi wowote ambao umewasilishwa na asasi yoyote ya umma kumhusisha na uovu huo.

Akijitetea mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi Jumapili, gavana huyo wa zamani wa Mombasa alieleza kuwa wakati mmoja, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa George Saitoti aliwasilisha ripoti bungeni ambayo ilimwondolea lawama kuhusu madai kuwa alihusika katika sakata ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

“Ni kweli kwamba madai hayo yamewahi kutolewa dhidi yangu. Uchunguzi ulifanywa na asasi husika za serikali. Baadaye aliyekuwa waziri wa usalama marehemu Saitoti aliwasilisha bungeni ripoti hiyo ya uchunguzi ulioendeshwa na asasi za humu nchini na kimataifa na hakukuwa na ushahidi wowote wa kunihusisha na madai hayo,” Bw Joho akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Alikuwa akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Teso Kusini Mary Emase aliyemtaka aieleze kamati hiyo endapo madai kwamba yeye ni mmoja wa walanguzi wa dawa za kulevya ni kweli au la.

Bw Joho alisema yeye hufanya biashara halali inayohusisha uchukuzi wa bidhaa na “endapo nilikuwa nikifanya biashara haramu singesazwa na serikali zilizopita.”