Habari Mseto

Mama ajiua kwa kukosa karo ya mwanawe

January 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BONIFACE MWANIKI

MWANAMKE wa miaka 37 alijitia kitanzi Jumatano asubuhi katika Kaunti ya Kitui baada ya kukosa karo ya kumpeleka bintiye kujiunga na kidato cha kwanza.

Majirani walisema mama huyo kutoka eneo la Kavisuni katika kaunti ndogo ya Katulani, aliamua kuchukua uamuzi huo pale alipoona watoto wengine wameshajiunga na shule za upili, huku bintiye akiwa nyumbani bila usaidizi.

Afisa Mkuu wa Polisi wa Utawala wa Katulani, Bw Alphonce Anaswa alisema msichana huyo alipata alama 396 na kuitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Chogoria iliyoko Kaunti ya Tharaka Nithi.

Alifanya mtihani wa KCPE katika shule ya msingi ya umma ya Mandongoi.

“Tulipashwa habari za kifo hiki leo asubuhi na jirani yake mama huyu. Aliupata mwili wake ukiwa umening’inia juu ya mti bomani mwake,” alisema Bw Anaswa.

Kulingana na afisa huyo wa polisi, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa huenda mama huyo alichukua hatua hiyo baada ya kukosa kupata karo ya shule ya msichana wake aliyefanya vyema katika mtihani wa darasa la nane mwaka jana.

Habari zilizopashwa polisi ni kuwa, msichana huyo alikuwa ametishia kujitia kitanzi iwapo mamake hangempeleka shule, hivyo hii huenda ikawa ndiyo sababu kubwa ya mama huyo kujitia kitanzi.

“Majirani walisema kuwa mtoto alikuwa ametishia kujiua endapo mamake hangepata karo yake ya shule. Lakini wanasema mama mwenyewe hakuwa na uwezo wa kupata pesa zinazohitajika kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya upili ya kitaifa,” akasema Bw Anaswa.

Kawaida shule za upili za bweni hutoza karo ya kuanzia Sh26,000 katika muhula wa kwanza. Hata hivyo, kuna mahitaji ya kimsingi kama vile sare za shule, vitabu, sanduku, usafiri na pesa za matumizi, ambazo pamoja na karo zinaweza kufika hata Sh60,000.

Haikufahamika mara moja kama mama huyo alikuwa amejaribu kutafuta usaidizi wa karo mahali popote. Maeneo Bunge na hata baadhi ya kaunti huwa na mpango wa basari kwa watoto werevu kutoka familia masikini.

Taifa Leo haikufanikiwa kujua ni kwa nini familia ya msichana huyo haikuomba usaidizi wa fedha, na kama iliomba ni kwa nani na kwa nini msichana huyo kufikia leo hajajiunga na shule ya upili alikoitwa.

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Umma mjini Kitui.