Habari Mseto

Mwanamke alivyoshambuliwa na fisi akaaga dunia papo hapo asubuhi

Na SIMON CIURI August 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMKE aliuawa na kundi la fisi Jumatano asubuhi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka sokoni.

Tukio hilo ndilo la hivi majuzi zaidi linalohusu binadamu kushambuliwa na wanyamamwitu ambapo kufikia sasa, watu watatu wameangamia na watano kujeruhiwa katika eneo la Juja Kusini, Kaunti ya Kiambu, katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Nancy Njoki Thuo, 52, ambaye ni mchuuzi wa vyakula, alikuwa anaelekea nyumbani kwake kuwaandalia wateja wake chakula aliposhambuliwa mwendo wa saa moja asubuhi.

Picha zilizoonekana na Taifa Leo zinaonyesha alijeruhiwa vibaya kichwani.

“Inahuzunisha kuwa aliaga dunia papo hapo na tunashirikiana na Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) kusaka fisi eneo hilo kwa sababu wamezidi kuzua hofu,” Kamanda wa Polisi, Juja, Michael Mwaura, alieleza Taifa Leo kupitia simu.

Wakazi eneo hilo wakiongozwa na Hellen Mukami na Allan Mburu walieleza wanahabari kuwa mkasa huo ungeliepukwa lau viongozi eneo hilo wangelishinikiza KWS kuwanasa fisi ambao wamekuwa wakirandaranda kote bila serikali kuingilia kati.

“Viongozi wetu wamekataa kusikiza kilio chetu. Hiki si kisa cha kwanza kwa sababu fisi wamewashambulia na kuwaua wanakijiji wengine wakiwemo watoto. Wengine wameachwa wakiuguza majeraha. Serikali ni sharti ichukue hatua kwa sababu tumechoka kulalamika pasipo hatua yoyote kuchukuliwa,” alisema.

Mapema mwaka huu, mtoto kwa jina Dennis Teya (10) aliuawa na kundi la fisi katika kijiji jirani cha Gwa Kigwi.

Wakazi wanasema wanahofia kuhusu usalama wa watoto wao shule zitakapofunguliwa katika muda wa wiki mbili zijazo.

Wanasema hali ya wachimbaji kware kukosa kuziba maeneo yaliyochimbwa na kukata vichaka, imevutia wanyamamwitu kwa kutoa sehemu salama za fisi kuzalishana na kujificha.

Maeneo yaliyoathirika zaidi Juja Kusini ni pamoja na Nyacaba, Witeithia, Maraba na Kabati, pamoja na Juja, Kaunti ya Kiambu.

Mapema mwaka huu, KWS ilisema kufikia sasa imehamisha fisi 12 kutoka Juja, katika juhudi za kupunguza visa vya binadamu kushambuliwa na wanyamamwitu eneo hilo.

KWS, kupitia taarifa, ilisema imetuma Kikosi cha Kudhibiti Kero la Wanyama (PAMU), ambacho kiliweka mitego katika sehemu mahsusi, kunasa fisi na kuongoza kikusi cha kutibu wanyama kuwahamisha fisi kutoka maeneo yanayosheheni binadamu.

“Inahuzunisha kuwa Kaunti ndogo ya Juja, Kaunti ya Kiambu, imeshuhudia ongezeko la visa vya wanyama kushambulia watu na kusababisha vifo. KWS inatuma risala za rambirambi kwa familia zilizoathirika,” ilisema KWS.