Joho anunulia kikosi chake ‘lunch’ baada kuapishwa rasmi kuwa Waziri
SAA chache baada ya kuapishwa kama Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, aliyekuwa gavana wa Mombasa, Hassan Ali Joho, alikutana na wabunge wote wa Pwani, maseneta pamoja na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir.
Katika kikao cha chakula cha mchana, viongozi hao isipokuwa mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, walijadiliana jinsi ya kuweka tofauti zao kando na kuboresha umoja.
Uteuzi wa Bw Joho kama waziri umeonekana kufufua umoja wa viongozi wa eneo hilo ambao walionekana kukosa kiongozi tangu Bw Joho, kuondoka katika ulingo wa siasa hatamu yake kama gavana ilipomalizika.
Viongozi waliochaguliwa kwa vyama vya ODM, UDA, Wiper Party na Pamoja Africa Alliance (PAA), walishiriki katika kikao hicho.
“Tulikutana kama viongozi na tumejadiliana jinsi ya kuungana na kudumisha umoja. Ni mengi tumejadiliana lakini siwezi kuyatangaza. Tutayaweka wazi hivi karibuni,” alisema mmoja wa wabunge walioshiriki chakula hicho cha mchana.
Mara ya mwisho kikao kama hicho kilifanyika, ilikuwa miezi tisa iliyopita ambapo Bw Joho ndiye alikuwa amekiitisha na walijadiliana masuala ya eneo la Pwani.
Bw Joho anayetambulika Pwani kama ‘sultani’ amekuwa kiungo muhimu katika siasa za Pwani kutokana na uwezo wake wa kushawishi viongozi kufuata mrengo fulani wa kisiasa.
Punde tu baada ya mkutano, viongozi walichukua fursa hiyo kumpongeza Bw Joho kwa nafasi hiyo yake mpya serikalini.
“Tuna furaha kuona Bw Joho akiapishwa kama Waziri wa Madini na tunamwambia tutashirikiana naye ili aweze kutekeleza kazi hiyo. Kulingana na weledi wake, hatuna shaka kuwa atatekeleza kazi hiyo,” alisema Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko.
Wakati viongozi hao wakikutana jijini Nairobi, katika kaunti sita za Pwani, amani ilidumu, huku vijana wakisusia maandamano wakisema kuteuliwa kwa Bw Joho na Bw Salim Mvurya katika baraza la mawaziri, ni dhihirisho kuwa wako kwa serikali.
“Kupewa wizara mbili na kuteuliwa kwa viongozi wetu mbalimbali serikalini kumetufurahisha hivyo tutaendelea kuomba Rais Ruto kutukumbuka siku zijazo,” alisema mkazi wa Mombasa, Bi Salima Hussein.
Hali shwari pia ilishuhidiwa katika kaunti za Kilifi, Tana River, Lamu, Taita-Taveta na Kwale huku vijana wenzao wakiandamana kupinga serikali ya sasa jijini Nairobi.