Jamvi La SiasaMakala

Azma ya Matiang’i kuvuruga karata za vigogo 2027

Na BENSON MATHEKA August 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ULINGO wa siasa nchini huenda ukabadilika pakubwa iwapo aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani, Dkt Fred Matiang’i, atajibwaga katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Yamkini kutakuwa na mazingira mapya ya kisiasa iwapo Dkt Matiang’i atadumisha uungwaji mkono ambao vijana wanaashiria kumpa.

Duru zinasema kwamba Dkt Matiangi ameanza kujiandaa  kugombea urais kwa kuajiri kampuni ya kimataifa kusuka mikakati ya kufanikisha azma yake.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kuna uwezekano atakuwa mwanasiasa anayemezewa mate na wagombeaji wengine wakitaka aungane nao.

Waziri huyo wa zamani anatambuliwa kwa misimamo yake mikali na maamuzi thabiti katika wizara tatu alizosimamia chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

 Japo amekuwa kimya, jina lake liliibuka katika kilele cha maandamano ya vijana kulalamikia gharama ya maisha na ufisadi serikali.

 Maandamano hayo yalipokuwa yakichacha, jina la Dkt Matiang’i,  ambaye  inasemekana anaishi ng’ambo liliibuka baadhi ya watumiaji wa mitandao wakimtaka  kujitokeza ili kujiunga nao kupigania uongozi bora na hata Rais wa Kenya 2027.

Vijana hao walisema kuwa Dkt Matiang’i alikuwa kiongozi aliyefanikiwa katika wizara mbalimbali alizosimamia.

“Matiang’i, mambo ni mawili: ujitokeze ama tuje tukuchukue. Tunahitaji uwe rais na si tafadhali,” Naomi Waithira aliandika kwenye mtandao wa X.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, iwapo umaarufu wake miongoni mwa vijana utadumu, Dkt Matiangi atakuwa mwanasiasa mwenye thamani kubwa katika uchaguzi mkuu ujao ikizingatiwa mikakati anayosemekana kutumia kujijenga na kujipigia debe.

 “Wanaofahamu mikakati ya siasa watakwambia kuwa jina la Dkt Matiang’i halikuibuka kwa bahati wakati  wa  kilele cha maandamano. Ni mkakati wa kutumia matukio yanayofuatiliwa na watu wengi kuwasilisha ujumbe ili ufikie watu wengi,” akasema mdadasi wa siasa Kephar Miruka.

“Akitumia mikakati kama hii bila kuchoka, na ikizingatiwa ushawishi na utendakazi  wake akiwa waziri ulioacha alama chanya  kwa Wakenya, basi atakuwa kama mwanamwali spesheli atakayewaniwa na wanasiasa wakitaka waungane naye katika uchaguzi mkuu wa 2027.”

Kulingana na mchambuzi huyu, Dkt Matiangi anaweza kunyima vigogo wa miaka mingi wa siasa kura za vijana kote nchini na za kaunti za Kisii na Nyamira na kuwa mfalme kivyake.

Hii ni ikizingatiwa kuwa viongozi wa mashinani katika kaunti hizo  wanamuunga mkono.

Rais William Ruto atatetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Kufikia sasa, ni kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye ametangaza azma ya kumpinga Rais Ruto.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga anagombea uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika ambao akishinda hataweza kugombea urais katika uchaguzi wa humu nchini.

Mwezi jana kakake, John Matiang’i alisema kuwa waziri huyo wa zamani  anafuatilia matukio ya siasa nchini.

 Bw  Miruka anasema  kwamba hata kabla ya maandamano ya vijana wa Gen Z dhidi ya serikali kuibuka, jina la Dkt Matiang’i lilikuwa vinywani mwa Wakenya.

“Anapendwa na Wakenya na zaidi ya yote na vijana ambao ndio idadi kubwa ya wapiga kura na wasio na ukabila. Hii pekee inakuonyesha kuwa ni mtu anayeungwa mkono na idadi kubwa ya wapiga kura na huyo ni mtu ambaye anaweza kuwatia tumbojoto wapinzani wake,” akasema.

Magavana Amos Nyaribo (Nyamira) na Simba Arati (Kisii), wamekuwa wakipigia debe kurejea kwa Dkt Matiang’i kwenye ulingo wa kisiasa.

“Tulikuwa na mtu wetu, Dkt Matiang’i, ninajua atakuja wakati unaofaa. Tutakuwa naye. Tuna viongozi wengine ambao watajibwaga uwanjani 2027. Tumedhamiria kuhakikisha kuwa siku moja, Omogusii (mtu wa jamii ya Abagusii) atakuwa kiongozi wa nchi,” akasema Bw Arati.

Wadadisi wanasema Matiang’i ana mtandao mkubwa wa marafiki aliounda akiwa waziri wa usalama wa ndani na ushirikishi wa serikali ya kitaifa ambao unaweza kufanya kupangua mikakati ya wagombeaji wengine wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ninachojua ni kwamba atamezea mate sana na viongozi wengine na vyama vya kisiasa  wakitaka ndoa ya kisiasa,” akasema mchambuzi  wa siasa Dkt Isaac Gichuki.