Makala

Ruto arudi ODM badala ya kusumbuana na Gachagua UDA

Na CECIL ODONGO August 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS Wiliam Ruto anastahili kumwachia Naibu Rais Rigathi Gachagua UDA na kujiunga na Kinara wa Upinzani Raila Odinga katika ODM ili kuhakikisha kuwa uchaguzi wa 2027 unakuwa mswaki kwake.

Kauli ya kila mara ya Bw Gachagua kuwa aliwekeza sana kwenye UDA katika uchaguzi mkuu wa 2022 hasa katika ukanda wa Mlima Kenya inasawiri jamii ya eneo hilo kama wanaomiliki chama hicho.

Akiwa katika Kaunti ya Kirinyaga wikendi, Naibu Rais alionekana kurejelea kauli hiyo akisema kuwa waliamka asubuhi na mapema kupigia utawala wa sasa kura na kwamba hawawezi kuondoka serikalini vivi hivi tu.

Aidha Bw Gachagua pia alinukuliwa akisema kuwa alishangazwa na kutimuliwa kwa aliyekuwa katibu mkuu Cleophas Malala kwa sababu hakuhusishwa ilhali yeye ni naibu kiongozi wa chama.

Mwanzo, mivutano ambayo imeanza kushuhudiwa ndani ya UDA inaashiria chama hicho kitakuwa na wakati mgumu 2027 hasa ukanda wa Mlima Kenya.

Kile ambacho ni dhahiri ni kuwa jamii ya Mlima Kenya haichangamkii utawala wa Rais Ruto hasa baada ya wandani wa Raila kuteuliwa serikalini.

Ingawa Bw Gachagua amekuwa akisisitiza kwenye mikutano ya umma kuwa ngome yake ya kisiasa ipo nyuma ya Rais, hiyo kwa sasa ni hadaa tupu.

Kwa kuwa ni kama eneo la Mlima Kenya lishamponyoka Rais kisiasa, anastahili kukumbatia ngome za Raila ambaye ameonyesha kuwa sasa yupo tayari kufanya kazi naye na kujijenga.

ODM ina umaarufu Pwani, Magharibi na Nyanza ikilinganishwa na UDA ambayo mabawa yake yamekuwa sana Bonde la Ufa na Mlima Kenya.

Kwa sababu kuna uwezekano finyu Raila atakuwa debeni 2027, ni vyema iwapo Rais atatumia mwanya huo na kurejea ODM, chama ambacho kilikuwa na umaarufu kila pembe ya nchi wanasiasa hao walipokuwa pamoja mnamo 2007.

Pili, katika uchaguzi wa 2027, Rais Ruto anahitaji tu ushindi wala umiliki wa chama hautakuwa hoja sana kwake hasa akishinda.

Iwapo Raila atafanikiwa kuwahi uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), basi itakuwa rahisi kwa Rais kudhibiti ODM na kutumia kura za ngome ya baba kujazia zile za Mlima Kenya.

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi tayari anaendeleza mchakato wa kuhakikisha kuwa ANC inajiunga na UDA kwa ajili ya 2027.

Kile ambacho Bw Mudavadi na Ruto wanastahili kufahamu ni kuwa iwapo Bw Gachagua atawaachia UDA, basi nia yao ya kutumia chama kimoja 2027 itakuwa ndoto.

Kama Rais atasalia na UDA iwapo Gachagua atagura, kisha Ruto asimamishe wawaniaji nao ODM pia waweke wagombeaji wao, vyama hivyo vitakuwa na ubabe usiofaa.

UDA ya Rais itaumia kwa kuwa itakuwa na uwezo finyu wa kushinda viti nje Bonde la Ufa huku ngome za ODM zikisalia nyuma ya chama hicho kwa sababu ya ushawishi wa Raila.

Kiongozi wa nchi atahitaji kuwa na wabunge wengi katika kura ya 2027 na hilo litatokea tu iwapo wanaomuunga mkono, wote watakuwa ndani ya ODM.

Jinsi Raila alivyomwokoa Rais kutoka kwa makali ya maandamano ya Gen Z ndivyo ataweza kumnusuru 2027 akitorokwa na Mlima Kenya lakini kiongozi wa nchi lazima arudi ODM.