Habari za Kitaifa

Utata waongezeka Raila akidai ni Uhuru alimwambia aongee na Ruto

Na CECIL ODONGO August 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga ameongeza utata kuhusu jinsi Serikali ilivyozima maandamano ya vijana, kwa kufichua kuwa ni Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aliyemwelekeza amtafute Rais William Ruto ili kutuliza Gen Z ambao walitishia kusambaratisha udhibiti wa nchi mwezi uliopita.

Katika kile ambacho sasa kinawaweka makatibu wa wizara mbalimbali roho mkononi, kiongozi huyo wa ODM amefichua kuwa alikuwa na makubaliano na Rais kuwa hata hao wafutwe kazi.

Bw Odinga amekuwa akikashifiwa na baadhi ya viongozi nchini kuwa aliyatumia maandamano hayo kujinufaisha kisiasa na kuwaingiza wandani wake serikalini.

Hata hivyo, waziri huyo mkuu wa zamani anasema ni simu aliyoipokea kutoka kwa Bw Kenyatta ndiyo ilisababisha asitishe msimamo wake mkali  dhidi ya serikali na kuongea na Rais ambaye aliridhia matakwa yake.

“Saa ile nchi inachomeka Uhuru ndiye alinipigia simu akaniambia nitafute Ruto niongee naye. Kenya ikichomeka itakuwa nchi nyingine mpaka tuzibe huu moto watu waketi chini waelewane,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa akiongea Jumanne katika eneobunge la Keiyo Kusini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet wakati wa mazishi ya Mzee Chirchir Masit, baba wa aliyekuwa Kamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) Irene Masit.

Bw Odinga alisema hakuitisha handisheki na Rais bali alimwambia waziwazi kuwa tatizo lililokwepo ni la uzembe na ukosefu wa uwajibikaji wa mawaziri wake.

 “William akanitafuta na mimi nikaongea naye wazi kabisa, nyinyi mnajua mambo yangu, sifichi mambo, nasema moja kwa moja. Ingawa magazeti yanaandika sijui nini Raila na Ruto wana handisheki, hakuna handisheki.

“Nikaongea na Ruto na nikaambia Ruto shida iko hapa. Hawa jamaa umewaweka pale hawajafanya kazi jinsi wananchi wanavyotaka.

Wananchi wameudhika na vijana ndio hawa wamejitokeza na wakaniambia baba wewe kaa nyumbani usitoke, umefanya ya kutosha wacha sisi tuendelee, hawa vijana si wendawazimu,” akaongeza Bw Odinga

“Hawa watu umewaweka pale wote hawajafanya ya kazi sawa sawa ndiyo maana hasira ni nyingi zaidi na hawa askari wako wanatumia nguvu zaidi wanapiga watu risasi watu ambao hawana silaha na hiyo inazidi kuleta hasira zaidi,” akasema.

Raila alikumbuka enzi alivyoshirikiana na Rais na Bw Kenyatta walipokuwa kwenye serikali ya muungano kati ya 2008-2013.  Wanasiasa hao watatu wote walikubaliana kuwa suluhu ya maandamano hayo ilikuwa lazima ipatikane kupitia mabadiliko serikalini.

 Alifunguka na kusema Rais alikubali pendekezo lake la kuwatimua mawaziri na makatibu wakuu ili serikali ianze upya katika kutimiza ajenda yake kwa raia.

“Shida iko hapa watu waketi chini waongee, akasikia (Ruto) na akasema mimi hawa mawaziri wataenda nyumbani nitawatoa. Nikasema hata hao makatibu wako hapo ni uchafu wote, wasafishe wote ili kuwe na watu wapya,” akasema Raila.

Waziri huyo mkuu ambaye mrengo wake ulinufaikia uteuzi wa mawaziri watano katika utawala wa sasa, alisema kuwa wakati umefika wa nchi kuandaa kongamano la kusuluhisha changamoto ambazo zimekwepo kwa miaka mingi.

“Watu wawe na kongamano ambalo tulikuwa nao hapo mbele na kuna mambo hayakusuluhishwa. Nataka tuwe na kongamano kupata nafasi ya kusuluhisha hayo mambo yote,”

Wakati wa mazishi hayo, Raila alilakiwa na wandani wa Ruto akiwemo Gavana wa Elgeyo Marakwet Wesley Rotich na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi.

Kauli ya Bw Odinga pia inawaweka vinara wenzake ndani ya Azimio pabaya kwa kuwa imekuwa ikidhaniwa wana baraka za Bw Kenyatta katika kupinga ushirikiano wa Raila na Ruto.