Charlene Ruto ataka umma ukome kumlimbikizia Rais matarajio yote ya maisha bora
BINTIYE Rais William Ruto, Charlene Ruto, ametoa changamoto kwa viongozi kuwajibikia utawala bora katika ngazi ya kaunti badala ya kuweka matarajio yote ya umma kwa Rais.
Akizungumza mjini Mombasa wakati wa sherehe za kitaifa za kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana mwaka huu, alidokeza kuwa vijana nchini Kenya hawafahamu hatua zilizowekwa na serikali ya kitaifa kwa manufaa yao hivyo basi kuwasababishia kufadhaika.
Alisema pengo kubwa lililopo katika kuarifu umma kuhusu shughuli za serikali zinazolenga vijana ni changamoto kubwa inayohitaji kutatuliwa.
“Viongozi katika kaunti, magavana, wanafaa kuchukua jukumu la kuwahudumia wapigakura wao.
“Rais wetu hivi majuzi alianzisha tovuti ya Ajira ambapo fursa zipo, kuna mambo mengi yanatokea karibu na sisi, lakini vijana hawayafahamu. Ni jukumu lako kufuatilia na kuweka juhudi,” alisema.
Charlene pia alisisitiza haja ya ushirikiano kati ya viongozi wa jamii, vijana, wawekezaji wa kibinafsi ili kuleta mabadiliko katika jamii.
Katibu wa Wizara ya Vijana, Bw Ismail Maalim Madey, alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika nafasi muhimu zaidi za maamuzi.
Hafla hiyo iliyoleta pamoja wawakilishi wa vijana kutoka kaunti zote 47 iliandaliwa Jumatatu katika kituo cha Swahilipot Hub mjini Mombasa.
Sherehe za wiki nzima katika kaunti zote zitatoa fursa kwa vijana kujihusisha na mipango ya serikali ya kaunti na ya kitaifa.
Bw Madey aliangazia ushirikiano na wadau mbalimbali ambao wameunga mkono juhudi hizi, hasa katika sekta ya dijitali na michezo.
“Tunahakikisha kwamba vijana wanaweza kuchuma riziki kutoka kwa ujuzi wao kupitia Talanta Hela,” alisema PS Madei, akizungumzia mpango huo unaolenga kukuza vipaji katika tasnia ya michezo na ubunifu.
Alisema vipaji 2,000 vimeibuliwa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Vijana na Elimu, ambapo vijana sita sasa wanacheza soka katika klabu za kimataifa.
Seneta Maalumu wa Mombas, Bi Miraj Abdillah, alitoa wito wa kupunguziwa ushuru kwa vijana wanaoanzisha biashara katika kaunti ili kuwasaidia kuanzisha msimamo thabiti.
“Tuwape muda vijana wanaoanza biashara, tusiwakatishe tamaa vijana wanaoanzisha biashara na mizigo ya kodi, wapate ahueni,” alisema na kuahidi kumshirikisha Mwenyekiti wa Baraza la Magavana. Anne Waiguru, kusaidia katika suala hili.
Hafla hiyo ilisisitiza juhudi za pamoja za wadau mbalimbali kuhakikisha vijana sio tu wanasherehekewa bali wanashiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wa taifa.