Habari za Kitaifa

Karibuni Eldoret, Jiji la Mabingwa!

Na BARNABAS BII August 15th, 2024 2 min read

MJI wa Eldoret, almaarufu kama Nyumbani kwa Mabingwa, sasa ni Jiji la Mabingwa nchini baada ya Rais William Ruto kuupandisha hadhi kuwa jiji.

Mji huo ambao ni makao makuu ya Kaunti ya Uasin Gishu umejiunga na kilabu cha majiji na sasa ndilo jiji la tano nchini baada ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru.

Ukiwa kusini mwa milima  Cherangani, mita 2,100 juu ya bahari,  miji huo ulitwikwa hadhi hiyo katika tamasha iliyojaa mbwembwe iliyoandaliwa Eldoret Sports Club.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, mawaziri kadhaa, viongozi wa Kaunti ya Uasin Gishu, wanariadha walioshiriki mashindano ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa na maelfu ya Wakenya, walihudhuria hafla hiyo.

Kabla ya hafla hiyo, Dkt Ruto alishiriki kikao  na wanariadha walioshiriki mashindano ya Olimpiki katika Ikulu ndogo ya Eldoret ambapo wote walioshinda medali walitunukiwa zawadi za pesa taslimu.

Kiongozi wa Taifa kisha aliongoza msafara kutoka Ikulu ndogo  hadi Eldoret Sports Club ambapo sherehe ya kukweza mjini huo wa viwanda Kaskazini mwa Bonde la Ufa, hadhi ya kuwa jiji jipya la Kenya.

Kabla ya kutangaza hatua ya kuinua hadhi ya Manispaa ya Eldoret kuwa Jiji la Eldoret, Rais Ruto alitia saini kuwa sheria mabadiliko kuhusu hadhi ya jiji huku Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Kosgei akimkabidhi mhuri na vifaa vingine vya mamlaka, Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu.

Rais  alikabidhi mfano wa vifunguo 14 kuashiria kaunti za Magharibi mwa Kenya, zilizo karibu na jiji jipya.

Kaunti hizo zinatazamiwa kunufaika  na maendeleo ya kijamii na kiuchumi baada ya mji wa Eldoret kupandishwa cheo kuwa jiji.

Aidha, Rais alitumia hafla hiyo kutuza watu kadhaa medali za kitaifa kwa kuchangia Eldoret kukua na kupanuka kufikia hadhi ya jiji wakiwemo wanariadha, wakulima na wafanyabiashara mashuhuri.

Miongoni mwao ni pamoja na marehemu Ezekiel Barngetuny na mwanariadha Vivian Cheruiyot waliokabidhiwa tuzo la Order of Burning Spear.

Meya wa zamani Joseph Lesiew ni miongoni mwa waliotuzwa Tuzo ya Order of Grand Warrior of Kenya.

Safari ya kuinua mji wa Eldoret kuwa jiji ilianza na pendekezo lililowasilishwa na Bodi ya Manispaa ya Eldoret, Mei 23, 2023.

Mnamo Januari 23, 2024, Seneti iliidhinisha kwa pamoja ripoti iliyowasilishwa na timu ya Bunge la Kitaifa ikipendekeza manispaa ya Eldoret kupandishwa hadhi kuwa jiji.

“Kamati inapendekeza Manispaa ya Eldoret itunukiwe hadhi ya jiji baada ya kutimiza masharti yanayohitajika chini ya Kipengee 5 na Awamu ya Kwanza ya Sheria kuhusu Miji na Majiji, 2011,” ilisema timu hiyo.