Habari za Kitaifa

Ruto achokoza Gen Z kwa jaribio la kurejesha mswada tata wa Fedha 2024 uliokataliwa

Na BRIAN AMBANI NA CHARLES WASONGA August 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

BAADHI ya wadau wamepinga mpango wa serikali wa kurejesha baadhi ya mapendekezo katika Mswada wa Fedha wa 2024 uliotupiliwa mbali Juni 28 kufuatia maandamano ya vijana wa Gen Zs.

Rais William Ruto Jumamosi, Agosti 17, 2024 alidokeza kuwa serikali inalenga kurejesha baadhi ya sehemu za mswada huo ili kuisadia serikali kupata angalau Sh130 bilioni za kufadhili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara.

Naye Waziri wa Fedha John Mbadi amedokeza kuwa wizara yake itarejesha pendekezo la utozaji ushuru wa mazingira kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje (Eco levy), kama mswada maalum.

Kauli hizi za Rais Ruto na Waziri Mbadi zimewafanya wadau katika sekta mbali kuingiwa na wasiwasi kwamba ni kisingizio cha kurejeshwa kwa baadhi ya mapendekezo ya ushuru yatakayoumiza wananchi.

Chama cha Wauzaji Magari yanayotumia Stima Nchini (Emak) ndicho cha kwanza kuibua hofu hiyo, kikisema kurejeshwa kwa ushuru kwa sekta hiyo kutayumbisha ununuzi na matumizi ya magari ya kutumia kawi hiyo (EVs).

Mwenyekiti wa chama hicho Hesbon Mose ameelezea hofu kwamba serikali itarejesha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya asilimia 16 kwa mabasi na pikipiki zinazotumia stima uliopendekezwa katika Mswada wa 2024.

Mswada huo pia uliondoa msamaha waVAT kwa vifaa vinavyotumiwa kuzalisha kawi kutokana na upepo na jua.

“Wakati huu bei ya magari yanayotumia stima (EVs) ni kati ya asilimia 10 na asilimia 15 ghali, ikilinganishwa na magari yenye injini ya kutumia petroli na dizeli (ICEs). Ukianzisha ushuru wa VAT na aina zingine za ushuru kwa EVs, bei ya magari hayo itaongekeza kwa asilimia 35 kuliko magariya ICEs,” akasema Bw Mose.

Aliongeza kuwa sekta hiyo, ya magari yanayotumia stima, ilivutia uwekezaji wa kima cha Sh13 bilioni mwaka jana, 2023, akisema kiwango hicho kitashuka ikiwa ushuru wa VAT utaanzishwa.

“Kati ya mwaka wa 2022 na 2023, tulishuhudia nyongeza ya asilimia 500 katika ununuzi wa pikipiki kwa sababu vyombo hivi vya usafiri havikutozwa ushuru wa VAT au aina nyingine za ushuru. Kurejesha ushuru huu katika sekta hii kutadumaza ukuaji wake na uwezo wake wa kutoa nafasi za ajira,” Bw Mose akasema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha Waagizaji Bidhaa na Wafanyabiashara Wadogo Nchini (ISTA) Samuel Karanja amepinga mpango wa Waziri wa Fedha John Mbadi wa kurejesha ushuru kwa bidhaa zilizopakiwa kwa plastiki na vitu vingine vinavyoharibu mazingira.

Kulingana na Bw Karanja, kurejeshwa kwa ushuru wa “Eco Levy) kutachangia kuongezeka kwa bei ya bidhaa nyingi za kimsingi.

“Bidhaa zinazotumika nchini na raia wa kawaida ni zile zilizoagizwa kutoka ng’ambo na ambazo hupakiwa kwa vifaa vinavyoathiri mazingira kama vile plastiki. Kwa hivyo, ikiwa Waziri Mbadi atarejesha ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zilizoagizwa nje, bei ya bidhaa hizo zitapanda. Hatua hiyo bila shaka itaongeza gharama ya maisha,” Bw Karanja akaambia Taifa Dijitali kwa njia ya simu.

“Kurejeshwa kwa ushuru huo kutachangia kuongezeka kwa gharama ya maisha na mahasla ndio wataumia,” akaongeza.

Lakini Bw Mbadi anashikilia kuwa kujeshwa kwa ushuru wa “Eco-levy) kutaisaidia serikali kupata pesa za kufadhili mipango ya utunzaji mazingira.

“Ikiwa bidhaa zinazoingizwa nchini zimepakiwa vitu kama plastiki zinazoharibu mazingira, sharti tutafute pesa za kuzuia uharibifu huu,” Bw Mbadi akasema Jumatatu, Agosti 19, 2024 kwenye mahojiano na wanahabari afisini mwake.

Akiongea katika eneo bunge la Malava, Kaunti ya Kakamega, Rais Ruto alielezea wazi nia ya serikali yake kurejesha baadhi ya mapendekezo ya mswada wa Fedha uliokataliwa, kuhusu ushuru, ili kupata pesa za kufadhili miradi ya maendeleo.

“Ingawa Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ungetusaidia kupata Sh347 bilioni, hatutakufa moyo. Tutarejea bungeni tena na kuwasilisha mapendekezo ya kutusaidia kupata pesa za kutusaidia kutekeleza miradi ya maendeleo. Kama mzazi, ikiwa unapanga kupata mtoto lakini kwa bahati mbaya mimba ikaharibika, hauvunjiki moja, unajaribu tena. Nimemwambia Bw Malulu (mbunge wa Malava Malulu Injendi) na wabunge wetu kwamba tutarejea bunge na mapendekezo kadhaa ya kutuwezesha kupata pesa za kujenga barabara na kuunganisha stima,” Dkt Ruto akasema.

Wakati huo huo, Wakenya wanafaa kujiandaa kwa kupanda kwa bei ya chakula kufuatia uamuzi wa Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) kuanza kutekeleza ushuru wa asilimia mbili (2) kwa bidhaa za chakula zilizoagizwa kutoka nje kama vile mahindi na mchele.

AFA imepuuza kilio cha wafanyabiashara wanaopinga hatua hiyo wakisema itaongeza gharama ya kuendesha biashara ya bidhaa za chakula, kando na kufanya bei ya bidhaa hizo kuwa ghali mno.