Habari za Kitaifa

Raila asusia mkutano wa Uhuru, tukio lililoonyesha huenda ukuruba umeshaisha

Na JUSTUS OCHIENG’ August 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa upinzani Raila Odinga Jumatatu aliongoza ODM kususia mkutano wa Baraza Kuu la Azimio la Azimio, kikao kilichostahili kuongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Tukio hilo sasa linaweka bayana kuwa huenda ukuruba wa kisiasa kati ya Bw Kenyatta na Raila katika uchaguzi mkuu wa 2022, umeisha na huenda kila moja ataenda njia zake mnamo 2027.

Mkutano wa baraza la Azimio ulikuwa uandaliwe saa 10 jioni na kuongozwa na Bw Kenyatta ambaye ni Mwenyekiti wa muungano huo. Hata hivyo, mambo yalibadilika baada ya ODM kuitisha kikao kingine na wanahabari na kutoa onyo kali dhidi ya Raila kutemwa Azimio.

Wawakilishi wa Wiper, DAP-Kenya, Kanu na PNU walikuwa tayari kwa mkutano huo ambao ulikuwa uandaliwe kupitia mtandao wa Zoom.

Hata hivyo, Narc Kenya ambayo kiongozi wake Martha Karua alishatangaza kuwa anaondoka Azimio na ODM haikuwa imethibitisha kuwa wangehudhuria kikao hicho.

‘Kuchezea kaa la moto’

Badala yake, ODM ikiongozwa na mwenyekiti wake Gladys Wanga (Gavana wa Homa Bay) waliitisha kikao na wanahabari ambapo walisema kuwa hawakuwa na ufahamu kuhusu mkutano huo. Isitoshe walionya dhidi ya jaribio lolote la kumbandua Raila kama kiongozi wa Azimio wakisema ni kama ‘kuchezea kaa la moto’.

Katika kile kilichoonekana kama ‘kiburi’ cha ODM, Bi Wanga pia alisema kuwa ni Katibu wa Azimio Junet Mohamed ndiye ana mamlaka ya kuitisha mkutano wa muungano huo wa upinzani.

Bw Mohamed ni mwandani wa Raila na Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Kitaifa.

Kinara wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa ambaye alikuwa tayari kwa mkutano huo alisisitiza kuwa Mabw Odinga na Mohammed walikuwa wakifahamu kuwa mkutano huo ulikwepo lakini wakaususia na kuusambaratisha.

“Mchana huu tulikuwa tuwe na mkutano wa baraza la Azimio ambao ulikuwa uongozwe na Uhuru Muigai Kenyatta. Sote tulialikwa na mkutano ulikuwa uanze saa 10 jioni lakini wenzetu wa ODM nao wakati huo wakaitishia kikao na kukashifu baraza la Azimio,” akasema Bw Wamalwa.

“Kwa hivyo, mkutano huo haukufanyika. Hii ina maana kuwa kila chama sasa kimeachwa kuamua mustakabali wake kuhusu kusalia au kuondoka Azimio jinsi ODM wamefanya,” akaongeza.

Jaribio la ‘kumtimua’ Raila Azimio

Katika kikao na wanahabari, ODM ilionya kuhusu jaribio lolote la kumpindua Raila Azimio. Kinara wa Wiper  Kalonzo Musyoka alifichua kuwa Bw Kenyatta angeongoza mkutano kuamua mustakabali wa uongozi wake baada ya wanachama watano wa  ODM kuteuliwa serikalini.

“Tulitarajia Uhuru ambaye ni mwenyekiti wa Azimio aongoze mkutano huo ili tujadiliane kuhusu changamoto zinazingira muungano wetu,” akasema Bw Musyoka.

Hata hivyo, Bi Wanga na Naibu Kiongozi wa ODM Geodfrey Osotsi ambaye pia ni Senata wa Vihiga, alisema kuwa mkutano wowote wa Azimio lazima ushirikishe ODM ili uwe na uzito.

Bw Osotsi alitoa onya kali kuwa jaribio lolote la kuandaa mkutano wa Azimio ili kumtimua Bw Odinga, utakumbana na vizingiti na adhabu kali kwa waliohudhuria.

“Ni Katibu Mkuu Junet Mohamed ndiye ana mamlaka ya kuitishia mkutano na hajafanya hivyo. Wakiendelea na kuwa na mkutano basi utakuwa wa kunywa chai au ule wa kangaroo na sio wa Azimio,” akasema Bw Osotsi.

Mgawanyiko unaojihidhirisha wazi unatokea tu baada ya Bw Odinga wiki jana kudai ni rais huyo mstaafu ndiye alimpigia simu aridhiane na Rais William Ruto.

Akiwa katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Raila alisema alisukumwa na Uhuru kuchukua hatua hiyo ili kutuliza nchi wakati ambapo maandamano ya Gen Z yalikuwa yameteka nchi mwezi uliopita.

-Imetafsiriwa na CECIL ODONGO