Habari Mseto

Bwanyenye Devani huru kwa dhamana ya Sh20 milioni katika kesi ya kulaghai benki Sh7.6 bilioni

Na RICHARD MUNGUTI August 20th, 2024 1 min read

MFANYABIASHARA bilionea Yagnesh Devani aliyekwepa mkono mrefu wa sheria miaka 15 alipokuwa ametorokea Uingereza, Jumatatu, Agosti 19, 2024 aliachiliwa kwa dhamana ya Sh20 milioni baada ya kukaa gerezani siku 13.

Devani alizuiliwa katika gereza la Viwandani, Nairobi baada ya kukanusha mashtaka ya kuifuja Benki ya Kenya Commercial 2008 ilipofadhili kampuni ya Triton Oil ununuzi wa mafuta ya ndege kwa thamani ya mabilioni ya pesa.

Devani, mmiliki wa Kampuni ya Triton Oil, aliyetiwa nguvuni Ulaya na kurudishwa nchini na polisi wa kimataifa Machi mwaka huu, 2024, alisukumwa gerezani Agosti 7, 2024 baada ya kukana mashtaka ya ulaghai na wizi wa Sh7.6 bilioni, katika kashfa ya mafuta ya ndege katika mabomba ya Kipevu, Kaunti ya Mombasa mwaka wa 2008.

Devani alikana aliilaghai Kenya Commercial Bank (KCB) mabilioni hayo.

Ni KCB iliyokuwa imeidhamini Triton mkopo wa kuwekeza katika biashara hiyo ya mafuta.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kupitia kwa wakili wa serikali Jeremiah Walusala aliambia mahakama, Devani aliuza mafuta hayo yaliyokuwa yanamilikiwa na KCB.

Aliposhtakiwa Agosti 7, 2024 Bw Walusala alipinga Devani kuachiliwa kwa dhamana akisema “atatoroka jinsi alihepa kizimba kwa miaka15.”

Lakini hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Thomas Nzioki alimwachilia Devani kwa dhamana ya Sh20 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi hicho, ama, alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh5 milioni.

Nzioki alisema ripoti ya idara ya urekebishaji tabia imewahoji watu wa familia ya mshtakiwa na wametoa ushuhuda ni mfanyabiashara aliyewekeza mali mengi na kwamba ameoa na yuko na mke na mtoto mmoja.

Hakimu alimwamuru mshtakiwa awasilishe pasipoti yake kortini na kumwonya ataona cha mtema kuni akivuruga mashahidi.

Kesi hiyo itatajwa manmo Agosti 29, 2024 kutengewa siku ya kusikizwa.