Raila alilia Wakenya wamuunge mkono kutwaa uenyekiti AUC, akinusia ushindi
KINARA wa Upinzani Raila Odinga amebashiri kuwa kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kitakuwa mswaki kwake baada ya azma yake kupokelewa vyema na marais wengi wa Afrika.
Bw Odinga Jumatano, Agosti 21, 2024 alisema kuwa viongozi wa Afrika tayari wanaunga mkono azma yake na akawataka Wakenya wamuunge mkono na kumtia shime kwenye kampeni zake.
Waziri huyo mkuu wa zamani tayari amewasilisha stakabadhi zake za kampeni kwa Afisi Kuu ya AUC na sasa yuko tayari kuanza kampeni kabambe za kushinda uchaguzi wa umoja huo hapo Februari 2025.
“Ningependa kushukuru uongozi wa bara hili kwa kuonyesha kuwa una imani nami. Kwa Wakenya wenzangu, ninahitaji uungwaji mkono wenu,” akasema Bw Odinga.
Kiongozi huyo wa ODM alikuwa akizungumza katika afisi ya Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi eneo la Railways katikati mwa jiji la Nairobi Jumatano, Agosti 21, 2024.
Bw Odinga na Mudavadi, walikuwa wameitisha kikao cha wanahabari kuzungumzia azma yake na jinsi serikali inavyopanga kumfanyia kampeni.
Kinara huyo wa upinzani alisema kuwa iwapo atachaguliwa Februari mwakani, atamakinikia matatizo mengi ambayo yanaathiri Bara la Afrika.
“Afrika inakabiliwa na changamoto tele hasa katika sekta za afya na elimu na kuna haja ya kuzalisha mali na kutatua ukosefu wa ajira, ambalo ndilo tatizo kuu zaidi,” akaongeza Bw Odinga.
“Vijana wengi wanazama kwenye bahari ya Shamu wakihepa umaskini Barani Afrika ili kusaka mali Ulaya. Haya ni mambo ambayo hayastahili kufanyika,” akasema Bw Odinga.
Pia, kinara huyo wa muungano wa Azimio la Umoja aliahidi kuimarisha sekta ya kawi kwa kuwa ina rasilimali za kutosha mbali na kumakinikia masuala ya tabianchi ambapo nchi za Afrika zimelalamika kuwa hazina sauti wakati ambapo sera zinapitishwa na mataifa ya Ulaya.
Wakati wa kikao Odinga na Mkuu wa Mawaziri, Bw Mudavadi alisema Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua rasmi afisi kuu ya kuendesha kampeni zake kote Afrika, Jumanne wiki ijayo.
Ni katika kikao hicho ambapo Rais atazindua kampeni na kutoa mwongozo wa jinsi kampeni za Raila zitakavyoendeshwa ili kuhakikisha anafaulu katika azma yake.
“Hii haihusu azma ya Bw Raila pekee bali ni suala la nchi kwa sababu kiongozi wetu anawakilisha sauti ya Wakenya, tabia na matamanio yao kwa Afrika. Kwa hivyo, tusimame naye wala tusiachie serikali pekee jambo hili,” akasema Bw Mudavadi ambaye pia ni waziri wa Masuala ya Kigeni.
Baadhi ya wapangaji mikakati wa Bw Raila ambao wanatarajiwa kuwa katika afisi hiyo kuu, ni Balozi wa zamani wa Kenya nchini Amerika Elkana Odembo, Balozi Anthony Okara, Prof Makau Mutua, aliyekuwa Naibu Gavana wa Nyeri, Dkt Caroline Karuga na aliyekuwa Katibu wa IGAD Mahboub Maalim.
Katibu katika wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo, Dkt Korir Sing’oei, katibu katika wizara ya Masuala ya Kigeni na katibu katika idara ya Masuala ya Bunge na Ofisi ya Kinara wa Mawazir Aurelia Rono walihudhuria kikao hicho.
Alipoulizwa kuhusu bajeti ambayo imetengewa kampeni za Bw Raila, Bw Mudavadi hakutoa takwimu lakini akasema kuwa hela zitatumika katika safari za kumpigia chapuo Bw Odinga.