Lapsset: Miundomisingi duni yazua taharuki
BODI ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Maendeleo ya Uchumi wa Afrika (ECA), imeelezea wasiwasi wake kuhusiana na kuwepo kwa miundomsingi duni kwa mataifa wanachama wa Mradi wa Bandari ya Lamu na Uchukuzi wa Ethiopia na Sudan Kusini (LAPSSET) inayofaa kukwepwa.
Badala yake, bodi hiyo imezishauri nchi tatu wanachama ambazo ni Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia kujikita katika masuala ya miundomsingi bora ya kitaifa.
Akihutubu wakati alipoongoza kongamano la wadau wa LAPSSET lililofanywa eneo la Kililana, Lamu, Mkurugenzi wa Mkutano huo wa awamu ya nne, Bw Stephen Karingi aliyasisitizia mataifa husika kuwekana kipaumbele katika kufunga au kusitisha miundomsingi yote duni inayozunguka mradi wa Lapsset na kuangazia ile ambayo ni muhimu kwa sasa.
Miongoni mwa miundomsingi hiyo ni barabara duni na zenye hadhi ya chini isiyotimiza makadirio yatarajiwayo kwa barabara kuu za Afrika.
Barabara hizo ni zile ambazo ni nyembamba na pia haziwezi kustahimili mabadiliko ya hali ya anga.
Bw Karingi alitaja janga la mafuriko lililoshuhudiwa nchini ambalo liliishia kuharibu barabara na miundomsingi mingine ya LAPSSET kuwa suala linalofaa kutiliwa maanani katika kuboresha miundomsingi husika ya mradi huo mkuu.
Mkurugenzi huyo pia alishikilia haja ya nchi tatu wanachama kutenga fedha za kutosha ili kujengea miradi ya reli katika Lapsset.
Mradi huo wa reli ya kisasa ni miongoni mwa miradi tanzu ya LAPSSET kipaumbele hasa kwenye Programu ya Miundomsingi na Maendeleo ya Africa (PIDA).
“Tunapoweka kipaumbele masuala kama hayo, ninaamini tutajikita vyema katika kuifanikisha hiyo miradi yote inayozunguka LAPSSET na bandari ya Lamu kwa jumla, hivyo kuafikia kupanuka kwa uchumi wa kikanda,” akasema Bw Karingi.
Pia aliipa changamoto sekta ya kibinafsi na washirika wote wa maendeleo ya kiuanachama kutambua vilivyo uwezo wa LAPSSET katika kuleta maendeleo na ushirika wa kimaendeleo.
“Ipo haja kwamba wakati huu tujikite katika kuziunganisha kamati zote za kiufundi katika kuleta mawazo mema ya kuiendeleza LAPSSET,” akasema Bw Karingi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa LAPSSET, Bw Stephen Ikua alisifu ushirika uliopo wa mataifa wanachama, akisema ni kupitia hali hiyo ambapo miradi ya LAPSSET inasukumwa mbele.
Naye Gavana wa Lamu, Issa Timamy aliahidi ushirikiano wake na wadau wote katika kufanikisha mipango yote inayozingira bandari ya Lamu na LAPSSET kwa jumla.