Mkenya alivyojikuta jela baada ya kudungwa kisu na Mpalestina
MWANAFUNZI Mkenya anayesomea nchini Algeria amehukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani kwa tuhuma za kumdunga kisu mwanafunzi mwenzake Mpalestina katika chumba cha malazi.
Ian Koima Kiprotich,24, anayesomea Shahada ya Uzamili ya Usanifu katika Chuo Kikuu cha Constantine 3, alihukumiwa mnamo Jumanne Agosti 20 na mahakama ya Algeria katika kesi ambayo hakuwakilishwa na wakili yeyote.
Hata hivyo wanafunzi wa Kenya nchini Algeria, wamelaani hukumu hiyo wakisema Kiprotich alinyimwa haki, na wanataka haki itendeke.
Kulingana na mwanafunzi mmoja Mkenya ambaye aliomba tulibane jina lake, wawili hao waligombana na Kiprotich alidungwa kisu mara tano.
Alikimbizwa katika Hospitali ya Centre-Universitaire de Constantine akiwa katika hali mbaya na kulazwa kwa siku tatu chini ya uangalizi maalum.
Lakini aliporuhusiwa kutoka hospitalini, Kiprotich alishtuka kukamatwa na kushtakiwa kwa “kumshambulia” mwanafunzi wa Kipalestina na kuitusi familia yake.
“Alidungwa kisu mara kadhaa shingoni, pajani na tumboni na mwanafunzi Mpalestina na mara akaanguka chini huku akivuja damu nyingi na kupoteza fahamu,” alisema mwanafunzi huyo Mkenya.
Wanafunzi hao walisema wanafunzi watatu kutoka Malawi, Uganda na Tanzania walioshuhudia zogo hilo, walifika kumuokoa na kumkimbiza hospitalini.
“Nashukuru Mungu kwamba maisha ya mwenzetu yaliokolewa na wanafunzi hawa watatu. Alikuwa akivuja damu nyingi kama inavyothibitishwa na damu iliyotapakaa chumbani mwake,” mwanafunzi huyo Mkenya aliongeza.
Kiprotich hakumudu kupata wakili wa kibinafsi na aliomba wakili wa umma, lakini juhudi zake ziliambulia patupu.
Cha kushangaza ni kwamba, aliyemshtaki alipewa wakili wa umma mara moja kumwakilisha mahakamani, huku Kiprotich akipewa mkalimani shughuli za mahakama zilipokuwa zikiendeshwa kwa Kiarabu.
“Kiprotich alinyimwa haki. Alikuwa na mashahidi watatu tayari kutoa ushahidi. Alinyimwa haki kwa sababu hakuwa na muda wa kutosha na uwakilishi wa kisheria kuandaa utetezi wake,” alidokeza mwanafunzi huyo.
Aliongeza, “Mashahidi walikuwa tayari kutoa ushahidi kwamba Kiprotich alikuwa chumbani mwake wakati wa shambulio hilo. Lakini walitishiwa na mshambuliaji.”
Mwanafunzi mwingine wa Kenya, ambaye hakutaka jina lake litajwe pia, alisema shambulio hilo halikuchochewa.
“Kiprotich alikuwa chumbani mwake. Hakukuwa vita. Kiprotich amenyimwa haki. Aliyemshtaki ana historia ya utovu wa nidhamu”.
Mwanafunzi mwingine alidai kuwa wakati fulani wa kesi hiyo, vita vya Israel dhidi ya Gaza vilitajwa, huku wakili anayemwakilisha mwanafunzi huyo wa Kipalestina akisema kuwa Algeria inapaswa kuwatetea Wapalestina wanaoteseka katika vita vya Gaza.