Kibarua kinachosubiri wakuu wapya wa KTDA
MISURURU ya changamoto inamsubiri Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya MajaniChai (KTDA) aliyechaguliwa kwa mara nyingine, Enos Njeru na naibu wake mpya, Erick Chepkwony, katika sekta inayokumbwa na misukosuko.
Kibarua kinachomsubiri ni pamoja na kuwaunganisha wakurugenzi, kusaka soko jipya kwa mazao ya majanichai nchini, kupigia debe mageuzi chini ya Sheria inayohusu Majani Chai 2020 na kuimarisha mchakato bora wa uzalishaji kutoka shambani hadi kiwandani.
Wawili hao wamechaguliwa wakati ambapo Katibu wa Wizara ya Kilimo, Paul Ronoh amekiri kuwa, kwa miaka miwili, mabohari ya Soko la Mnada wa Majani Chai Mombasa, yamefurika mruundiko wa majani chai yanayosubiri kuuzwa.
“Baadhi ya majani chai yamerejeshwa kwenye ukumbi wa mnada mara 32 bila kuuzwa kutokana na bei ya akiba iliyowekwa na serikali. Ni suala tunaloangazia na wadau,” alisema Dkt Ronoh.
Alisema haya Jumamosi, Agosti 24, 2024 katika Kiwanda cha Majani Chai cha Tirgaga, Kaunti ya Bomet, ambapo alifichua kufikia sasa, kilo milioni 45 za majani chai zimeuzwa, kiasi kikubwa zaidi kuwahi kuuzwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“Tunaangazia vikwazo vinavyoathiri mauzo ya majani chai mnadani na kushughulikia jinsi ya kuunda masoko mapya kwa chai iliyoundiwa Kenya,” alisema Dkt Ronoh.
“Huku uzalishaji ukizidi kupanda kutokana na athari ya mbolea ya bei nafuu kwa wakulima 680, 000 hali shwari ya anga, serikali inasaka vituo vipya vya kuuzia mazao hayo.”
Wanasubiriwa pia na kibarua cha kuponya migawanyiko iliyosababishwa na chaguzi hizo zilizofanyika katika Hoteli ya Pride Inn, Shanzu, zilizosusiwa na wakurugenzi wengine saba akiwemo Mbunge wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe.
Bw Kagombe aliwaongoza wakurugenzi wenzake, Chege Kirundi, John Wasusana, James Omweno na Mwangi Githinji kupinga matokeo ya uchaguzi huo wakilalamikia kuingiliwa na Wizara ya Kilimo na Bodi ya Majani Chai Nchini.