Habari za Kitaifa

Oyuu ni msaliti, walimu wachemkia uongozi wa KNUT

Na WAANDISHI WETU August 27th, 2024 3 min read

BAADHI ya wanachama wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Jumatatu, Agosti 26, 2024 walilalamikia kile walichotaja kama usaliti wa viongozi wao wakuu waliofutilia mbali mgomo wao kabla ya serikali kutimiza matakwa yao yote.

Walimu hao walimshutumu vikali Katibu Mkuu wa chama hicho Collins Oyuu kwa kutangaza kuondolewa kwa notisi ya mgomo huo ambao ulipaswa kumalizika usiku wa kuamkia Jumatatu (Agosti 26, 2024).

“Binafsi nimevunjwa moyo na viongozi wetu wa KNUT, haswa Katibu Mkuu Collins Oyuu ambaye alitangaza kufutiliwa mbali kwa mgomo wetu ambao ulifaa kuanza Jumatatu. Bw Oyuu alitoa tangazo hilo hata kabla ya kutimiza matakwa yetu makuu kama vile kupandishwa vyeo kwa walimu, kuajiriwa kwa walimu wa JSS kwa mkataba wa kudumu na kuajiriwa kwa walimu wengine 20, 000 ili kutupunguzia mzigo wa kazi,” akasema John Kariuki ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Langa Langa, Gilgil, Kaunti ya Nakuru.

Kwa upande wake, Bw Cornelius Mukabana ambaye ni mwalimu katika shule ya Msingi ya Ronald Ngala, Dandora, Nairobi alidai kuwa viongozi wao “wametiwa mfukoni na serikali”.

“Bw Collins Oyuu na wenzao wamemeza ndoano ya serikali na ndiposa wakaamua kufutilia mbali mgomo. Wangekaa ngumu kama wenzao wa KUPPET ambao walitangaza kuendelea kwa mgomo,” akasema mwalimu huyo ambaye alikiri kuripoti kazini japo shingo upande.

KUPPET ni Muugano wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai.

Mnamo Jumapili jioni, Agosti 25, 2024 Bw Oyuu alitangaza kufutiliwa mbali kwa mgomo wa wanachama wa KNUT baada ya kuongoza mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi.

“Baada ya NEC kukadiria mambo yote kuhusu suala hilo na kiwango cha kujitoleaa kwa serikali na Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kushughulikia malalamishi ya wanachama wetu, leo (Jumapili) imeamua kuondoa notisi ya mgomo ambao uliratibiwa kuanza usiku wa kuamkia Jumatatu,” Bw Oyuu akasema kwenye kikao na wanahabari.

“Aidha, tumeshawishika kuwa baadhi ya malalamishi yaliyosalia yanaweza kukatatuliwa na serikali kwa ushirikiano na TSC kindani,” katibu huyo mkuu akaongeza.

Baadhi ya malalamishi ya KNUT yalikuwa kwamba TSC iwape ajira ya kudumu walimu 46, 000 vibarua wanaofundisha katika Shule za Upili za Msingi (JSS), iajiri walimu 20, 000 zaidi ili kupunguza kero ya uhaba wa walimu na mzigo kwa walimu wanaohudumu sasa.

Vile vile, KNUT ilikuwa ikiishinikiza TSC kuwapandisha vyeo zaidi ya walimu 130, 000 waliohitimu kufikia mwaka ujao, 2024.

TSC imekuwa ikijivuta kuanza shughuli ya kuwaajiri walimu hao licha ya serikali ya kitaifa kutangaza kuwa imetenga Sh18.7 bilioni za kugharamia shughuli hiyo.

Mnamo Jumapili jioni, Waziri wa Fedha John Mbadi alitangaza kuwa pesa hizo zipo na kwamba walimu wa JSS “wataanza kuajiriwa wakati wowote kuanzia sasa,”

“Ningependa kuondoa kauli yangu ya hapo awali kwamba serikali haina pesa za kuajiri walimu wa JSS. Pesa zipo na wakati wowote kuanzia sasa TSC itaanzisha mpango wa kuajiri walimu hao,” akaeleza.

Wakati huo huo, Jumatatu shule kadhaa za msingi zilifunguliwa kwa masomo ya muhula wa tatu lakini ni wanafunzi wachache waliripoti katika taasisi hizo.

Lakini nyingi za shule za upili zilisalia mahame baada ya walimu kususia kazi na kuamua kushiriki maandamano.

Hii ni baada ya chama cha kutetea masilahi ya walimu hao (KUPPET) kushauri wanachama wake, wengi wao wakiwa walimu wa shule za upili, kuanza mgomo.

Jumatatu, Waziri wa Leba Alfred Mutua alifanya mkutano na viongozi wa kitaifa wa KUPPET kujaribu kuwashawishi kufutilia mbali mgomo huo.

“Waziri alikubali kuwa matakwa yetu yana uzito na sasa atafanya mkutano na TSC. Hatuna haraka,” Katibu Mkuu Akello Misori akaambia Taifa Dijitali.

Mkutano huo ulianza saa tatu na nusu asubuhi (9.30am) na kuendelea hadi saa nane na dakika 45. Wakati wa mkutano huo, Dkt Mutua alikuwa akishauriana na Rais William Ruto, Waziri wa Elimu Julius Migos na Waziri wa Fedha Bw Mbadi.

Mkutano mwingine kati ya Waziri Mutua na viongozi wa KUPPET umepangiwa kufanyika kesho, Jumatano, Agosti 28, 2024.

Dkt Mutua alipokuwa akikutana na viongozi wa KUPPET, wanachama wake ambao ni walimu wa shule za upili, walifanya maandamano katika kaunti za Mombasa, Nyandarua, Kisii, Bomet, Kericho, Uasin Gishu, Makueni, Kilifi, Meru, Laikipia, Siaya miongoni mwa zingine wakishiniza TSC na serikali kutimiza matakwa yao.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga