Habari za Kitaifa

Korti yazima mgomo wa walimu

Na DAVID MCHUNGUH August 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Leba jijini Nairobi imesitisha mgomo wa walimu unaoendelea ulioitishwa na Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya mafunzo (Kuppet).

Jaji James Rika Jumanne, Agosti 27, 2024 alisema mgomo unasimamishwa hadi kesi iliyowasilishwa na Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) isikizwe na kuamuliwa.

“Hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa, agizo linatolewa kuzuia mshtakiwa (Kuppet), maafisa wake, wanachama, wafanyikazi, maajenti, au mtu mwingine anayefanya kazi kwa niaba yake, kugoma au kuanza kugoma, kujihusisha, kushiriki au kuendelea kushiriki mgomo ulioanza Agosti 2024 au wakati mwingine wowote baada ya hapo,” linasema agizo hilo.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 5, 2024.

Agizo hilo ni ushindi kwa TSC na Wizara ya Elimu ambayo imekuwa ikitaka shule zifunguliwe kwa muhula wa tatu bila kutatizwa na mgomo.

Walimu hao walianza mgomo wao Jumatatu, Agosti 26, 2024 na kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya wazazi wamechelewa kuwaachilia watoto wao kurudi shuleni kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu usalama wao shuleni.

Kuppet ina idadi kubwa ya wanachama ambao ni walimu wa shule za upili.