Habari Mseto

Afisa wa GSU akamatwa kwa kufyatulia mkewe risasi

Na HILARY KIMUYU August 28th, 2024 1 min read

AFISA Mkuu wa Polisi wa Kitengo cha GSU, Stephen Kiptanui Soi Jumanne, Agosti 27, 2024 alikamatwa kwa madai ya kumpiga risasi na kumjeruhi vibaya mkewe nyumbani kwao eneo la Ketete, Kaunti ya Narok.

Bw Soi, ambaye pia alihudumu kama afisa wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOCK), mnamo 2021 alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela au kulipa faini ya Sh103 milioni kwa kuhusika katika kashfa ya Olimpiki iliofanyika Rio 2016.

Inadaiwa alimpiga risasi na kumjeruhi mkewe, wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, nyumbani kwao Jumanne asubuhi kufuatia ugomvi.

Kulingana na polisi, Bw Soi anaruhusiwa kuwa na silaha aina ya bunduki.

“Mwathiriwa alijeruhiwa kwenye paja lake la mguu wa kushoto na alilazwa katika hospitali ya kibinafsi ya eneo hilo akiwa katika hali nzuri,” ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Mulot ilisema.

Polisi walisema walipozuru eneo la tukio, Bw Soi hakuwa ndani ya nyumba hiyo, jambo lililosababisha polisi kufanya msako mfupi wa kumtafuta pamoja na bastola aina ya Ceska iliyotumiwa katika tukio hilo.

Baadaye alipatikana na kukamatwa. Baada ya upekuzi katika nyumba hiyo, polisi walipata magazini likiwa na risasi 12.

Bunduki iliyotumika katika tukio hilo ilikutwa chumbani kwake ikiwa na magazini iliyokuwa na risasi sita.

Risasi iliyotumika pia ilipatikana kwenye eneo la tukio, polisi waliongeza.

Bunduki hiyo ilitumwa kwa uchunguzi wa silaha.

Polisi walisema Soi, 68, atashtakiwa kwa jaribio la kuua wakati uchunguzi utakapokamilika.

Vilevile, polisi pia wanachunguza mazingira yaliyosababisha afisa huyo kufyatua risasi.