Salah kimya kuhusu mipango yake
MSHAMBULIAJI wa Liverpool Mohamed Salah amesema kwa sasa analenga kucheza tu akifurahia kiwango chake huku akisubiri mkataba wake unaokaribia ukingoni utamatike ili azungumze kuhusu hali yake ya baadaye.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alikubali mkataba mpya kuendelea kuchezea Liverpool, lakini utamalizika baada ya msimu huu wa 2024/2025.
Septemba 2023, Liverpool ilikataa kumuachilia ajiunge na Al-Ittihad baada ya klabu hiyo kuweka mezani kiasi cha Sh25.4 bilioni.
“Sitaki kuzungumzia kuhusu mwaka ujao. Lengo langu kwa sasa ni kufurahia mwaka uliobaki kwenye kandarasi yangu, na baadaye niamue maisha yangu ya baadaye. Muhimu ni kuendelea kufanya kazi yangu ya kucheza soka,” alisema.
Salah alijiunga na Liverpool kwa mkataba wa Sh5.7 bilioni akitokea klabu ya AS Roma mnamo 2017 ambapo kufikia sasa ameifungia jumla ya mabao 213 katika mechi 351.
Anashikilia nafasi ya tano katika orodha ya wafungaji bora wa Liverpool.
Mnamo Julai 2022, mchezaji huyo alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu, uliomfanya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye klabu hiyo, akilipwa zaidi Sh59,462,897.79 kwa wiki.
Chini ya kocha mpya, Arne Slot, tayari staa huyo amefunga mabao mawili kwenye ligi kuu iliyoanza wiki mbili zilizopita.
Alisaidia klabu hiyo kushinda mataji yote makubwa, isipokuwa lile la Europa League chini ya kocha Jurgen Klopp aliyeondoka katika msimu wa 2013/2014.