Habari za Kitaifa

KUPPET tawi la Kilifi: Hatutatishwa, mgomo wa walimu unaendelea

Na JURGEN NAMBEKA August 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha walimu wa shule za upili na vyuo (KUPPET) tawi la Kilifi kimeeleza kuwa hakitashurutishwa na vitisho vya serikali kusitisha mgomo wao kabla ya matakwa yao kutekelezwa.

Wakizungumza na wanahabari baada ya maandamano yao, walisema kuwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) isingewasukuma kurejea madarasani bila ya kutekeleza ahadi zake kwa walimu.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama hicho tawi la Kilifi Bw Chiguba Nyale, walimu watashikilia msimamo huo hadi pale serikali itakapotimiza matakwa yao.

“Walimu ndio nguzo ya elimu humu nchini. Sisi hatuogopi na hatutatishwa na yeyote kukomesha mgomo. Tunaomba wadau wa sekta hii na wazazi mtuunge mkono katika vita hivi vya kutetea maslahi yetu,” akasema Bw Nyale.

Viongozi wa muungano huo waliwaonya walimu wakuu waliokuwa wakiwashurutisha walimu kurejea darasani kabla ya matakwa yao kutimizwa.