Habari Mseto

Afisa wa KDF taabani kuhusu hongo ya kuingiza vijana kwa jeshi

January 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa Jeshi Ijumaa alishtakiwa kwa kupokea zaidi ya Sh400,000 kutoka kwa makurutu waliokuwa wanachaguliwa kujiunga na Jeshi la Kitaifa (KDF).

Mahakama ilifahamishwa kuwa makurutu waliokuwa wamepewa barua za kujiunga na KDF walitimuliwa kutoka chuo cha kutoa mafunzo ya kijeshi cha Lanet.

Bw Calvin Amugune Amata almaarufu Captain mwenye umri wa  miaka 36 alikanusha mashtaka 10 aliposhtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Nairobi.

Bw Amata alishtakiwa kuwa kati ya Desemba 25 , 2018 na Januari 5, 2019 jijini Nairobi akishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani akiwa na nia ya kulaghai alipokea Sh425,000 kutoka kwa Bw Mwadama Bakari Mwalimu akidai atamsaidia kuandikisha wavulana wake wanne katika KDF.

Shtaka lilisema afisa huyo wa Jeshi alimdanganya Bw Mwalimu atamsaidia kuwaandikisha Mohammed Ali Nyaa, Rashidi Sudi Muchombo, Jeupe Ngozi Salimu Ndaro na Mwachikaha Hamisi Koma Koma katika idara ya KDF.

Mahakama iliambiwa mshtakiwa alijua alikuwa anamdanganya Bw Mwalimu.

Shtaka la pili lilisema mshtakiwa alijitambulisha kuwa afisa wa KDF mwenye cheo cha Captain.

Captain alishtakiwa kumpa Mwachikaha Hamisi Komakoma barua ya kujiunga na KDF nambari (S/No).1843432 akijifanya barua hiyo ilikuwa halisi iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi.

Alidaiwa alijitambulisha hivyo kwa makrutu kuwahadaa alikuwa na uwezo wa kuwaandikisha katika KDF.

Shtaka la tatu lilisema Bw Komakoma aliipeana barua hiyo kwa wizara ya Afya.

Mshtakiwa huyo alikabiliwa na shtaka la kughushi barua nyingine ya kujiunga na KDF na kumkabidhi Bw Muchombo akidai ni halisi iliyoandikwa na idara ya kijeshi.

Barua nyingine feki ilikabidhiwa Bw Ndaro na Bw Amata.

Mashtaka ya tisa na kumi yalisema kuwa  Bw Amata alighushi barua za kujiunga na KDF na kumpa Bw Nyaa.

Bw Amata , ambaye hakuwa amewakilishwa na wakili alimsihi hakimu amwachilie kwa dhamana akisem , “niko na watoto wanaonitegemea.”

Akarai , “Mheshimwa naomba uniachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu. Niko na watoto wanaonitegemea kujikimu kimaisha.”

Alisema anamsaidia mama yake Mzee na endapo atapewa dhamana ya kiwango cha juu bila shaka atasalia gerezani na familia yake itateseka.

Kiongozi wa mashhtaka Bw Kennedy Panyako hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Hakimu aliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000.

Kesi itasikizwa Feburuari 15, 2019 na kutajwa Januari 25 kwa maagizo zaidi.