Habari za Kitaifa

Ngilu akengeuka, sasa aunga Kalonzo na kupinga serikali

Na PAUL MUTUA September 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa Narc Charity Ngilu amekengeuka na sasa anamtaka Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aimarishe siasa zake na kujaza pengo lililoachwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kwenye upinzani.

Bi Ngilu katika kile kilichoonekana kubadilisha msimamo wake, alisema Raila amewataliki wafuasi wake waliompigania kwa kuungana na serikali akimtaka Bw Musyoka kuchukua nafasi hiyo na kuwaongoza Wakenya kusaka mabadiliko ya utawala nchini.

Alikuwa akizungumza katika kijiji cha Ngiluni, eneobunge la Kitui Mashambani ambapo alitaka jamii hiyo kuwa na umoja kwa sababu mawimbi makali yatakayoondoa uongozi wa sasa mamlakani yanakuja 2027.

Alisema utawala wa sasa umefanya maisha yakawa magumu ndiposa Wakenya wanahitajika kuwa na umoja na kukumbatia mabadiliko nchini.

‘’Tujiandae kwa vita vya kukomboa nchi yetu. Tusitarajie tu kuwa tutapewa urais, lazima tuungane na kusaka wadhifa huo,” akasema Bi Ngilu.

Kinaya ni kuwa chini ya wiki moja iliyopita, Bi Ngilu aliitaka jamii ya Wakamba kuunga mkono utawala wa sasa wa Rais William Ruto akisema ndiyo njia pekee ambayo itahakikisha wanapata maendeleo kabla ya kura ya 2027.

Akiongea katika mazishi ya Mzee Mwangangi Masila, 90 ambaye alikuwa mshirika wake wa kisiasa kwa miaka mingi, Bi Ngilu wikendi alimtaka Bw Musyoka aendelee kusaka uongozi kutoka maeneo mengine ya nchi ili kuwahi urais mnamo 2027.

Gavana huyo wa zamani wa Kitui alimwambia mbunge wa eneo hilo Bonny Mwalika amkumbushe Kalonzo kuwa safari ya kusaka urais si rahisi na itabidi ahakikishe wanaotoka ngome yake ya kisiasa wamejisajili kwa wingi kama wapigakura.