Habari za Kitaifa

Ziko wapi pesa zilizochangwa kwa kampeni za Raila AUC?

Na JUSTUS OCHIENG September 17th, 2024 2 min read

KUJITENGA kwa serikali na shughuli ya kuchanga  fedha kupiga jeki kampeni za Raila Odinga za kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kumeanika jinsi mipango ya kuratibiwa kwa kampeni ilivyovurugika.

Hatua hiyo imeibua maswali kuhusu uhalali wa shughuli za vuguvugu la Friends of Baba— Africa (FOBA), lililoasisiwa na binamuye Bw Odinga, Jaoko Oburu.

Kulingana na Bw Oburu, FOBA inaongozwa na mbunge wa zamani wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Mumbi Ngaru huku Mkurugenzi wake Mkuu akiwa ni Winnie Mandela- Rais wa Kundi la Kutetea Masilahi ya Afrika-Afrika na Ughaibuni.

Maswali yameibuliwa kuhusu dhifa hiyo ya chakula cha jioni iliyoratibiwa kufanyika Septemba 18 kuchangisha fedha za kufadhili kampeni za Bw Odinga.

Taifa Leo ilipomfikia Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei, ambaye pia ni mwenyekiti wa sekritariati ya kushirikisha kampeni za Odinga, kubaini ikiwa serikali ni mshirika katika mipango ya shughuli hiyo, alisema sekritariati anayoongoza haihusiki.

Baadaye Dkt Sing’oei aliweka taarifa fupi katika akaunti yake ya mtandao wa X akifafanua msimamo huo.

“Sekritariati ya kusimamia kampeni za Mheshimiwa Raila Odinga haihusiki na shughuli hii ya kuchanga fedha,” Katibu huyo akaandika mnamo Jumatano Septemba 11, 2024.

Aliyekuwa Balozi wa Kenya Amerika Elkanah Odembo ambaye ni miongoni mwa wapangamikakati ya kampeni za Bw Odinga pia alisema halifahamu kundi hilo linalopanga shughuli hiyo ya kuchanga fedha za kampeni.

“Tafadhali wasiliana nao kupitia nambari za simu walizoweka hapo na ubaini wao ni akina nani na nani aliwapa idhini ya kuandaa mchango huo,” Bw Odembo akaambia Taifa Leo.

Kulingana na mwaliko kwa dhifa hiyo inayotarajiwa kufanyika katika mkahawa mmoja wa kifahari jijini Nairobi, wageni kutoka Kenya na mataifa kadhaa ya Afrika wanatarajiwa kuhudhuria.

“Ungana nasi mnamo Septemba 18, 2024 jijini Nairobi, tunapoungana na viongozi na wageni wengine  kutoka nchi kadhaa za bara Afrika ili tusaidie kuendeleza mustabali bora wa Afrika,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya mwaliko.

Wageni wameshauriwa kuwasiliana na Bi Winnie Mandela na kupitia nambari nyingine ya simu iliyodaiwa kuwa yake Bw Oburu, ili kupata maelezo zaidi kuhusu shughuli hiyo.

Lakini tulipopiga nambari hiyo ya simu, ilitokea kwamba ni ya mtu mwingine wala sio Bw Oburu, ambaye ni mwanawe kakake Bw Odinga, Seneta wa Siaya Oburu Oginga.

Hata hivyo, Bi Mandela alithibitisha kuwa kundi la FOBA ndilo lililoandaa shughuli hiyo ya kuchanga fedha.

Hata hivyo, alisema kuwa asingetoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo “kwa sababu sina uwezo kufanya hivyo.”