Kimataifa

Zimbabwe kuchinja ndovu 200 kuokoa waathiriwa wa njaa


HUKU mataifa ya Afrika yakijizatiti kutunza wanyamapori, haswa ndovu, Zimbabwe inapanga kuwachinja ndovu 200 kulisha jamii zinazokabiliwa na baa la njaa.

Nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula kutokana na kiangazi kikali kuwahi kushuhudiwa nchini humo ndani ya miongo minne.

Kiangazi hicho, kilichojiri baada ya mvua kubwa ya El Nino, kimeharibu mimea ya chakula nchini Zimbabwe na kuathiri watu milioni 68 na kusababisha ukosefu wa chakula katika maeneo yote nchini humo.

“Tunaweza kuthibitisha kuwa tunapanga kuua ndovu 200 kote nchini kwa ajili ya nyama. Tunapanga  namna ya kutekeleza zoezi hilo,” msemaji wa Mamlaka ya Kusimamia Mbuga na Wanyamapori Zimbabwe (Zimparks) Tinashe Farawo, akaambia wanahabari.

Alieleza kuwa nyama ya ndovu hao itasambaziwa familia mbalimbali zilizoathiriwa na kiangazi nchini Zimbabwe.

Farawo hata hivyo alifafanua kuwa ni ndovu wa kiume waliozeeka ndio watalengwa katika shughuli kama hiyo iliyofanyika mara ya mwisho nchini Zimbabwe mnamo 1988.

“Zoezi hilo litaendeshwa katika wilaya za Hwange, Mbire, Tsholotsho na Chiredzi” akaeleza.

Hatua ambayo Zimbabwe imechukua inafuata ile ambayo ilichukuliwa na nchi jirani ya Namibia mwezi wa Agosti ambayo ilichinja ndovu 83 na kusambaza nyama kwa waathiriwa wa kiangazi.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya ndovu 200,000 wanaishi katika maeneo ya uhifadhi katika nchi tano za Afrika Kusini, ambazo ni Zimbabwe, Zambia, Botswana, Angola na Namibia.

Kwa hivyo, eneo hilo linatambuliwa kama lenye idadi kubwa zaidi ya ndovu duniani.

Farawo alisema shughuli hiyo ya kuchinja ndovu ni sehemu za juhudi za kupunguza msongamano katika mbuga zake za wanyama, ambazo zina uwezo wa kusitiri ndovu 55,000 pekee.

Kwa ujumla Zimbabwe ina jumla ya ndovu 84, 000.