Makala

Raila alivyozima siasa za urithi ndani ya ODM


KATIKA kile kinachoweza kutajwa kama kuwaua ndege wawili kwa kutumia jiwe moja, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alitumia mwafaka kati yake na Rais William Ruto kuzima mivutano kuhusu urithi iliyotishia kugawanya chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM).

Hatua hiyo ilimwezesha kupenyeza ndani ya serikali na hivyo kuweza kupata uungwaji mkono anapowania wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kabla ya vijana wa Gen Z kuanzisha maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 Juni 18 na Rais Ruto kuwafuta kazi mawaziri wake 21, wandani wa Bw Odinga walikuwa wameanzisha kampeni ya kutaka kurithi wadhifa wa kiongozi wa ODM.

Hii ni baada ya Waziri huyo Mkuu wa zamani kutangaza mnamo Februari 15, nia yake ya kuwania kiti hicho baada ya Moussa Faki Mahamat kustaafu Februari 2025.

Licha ya Bw Odinga kutoa wito kwa viongozi hao kusitisha kampeni za kurithi wadhifa wake, kampeni ziliendelea kambi tofauti zikichipuka zikiegema wawaniaji mbalimbali.

Ilihofiwa kuwa kampeni hizo zingetishia umoja katika ODM.

Wale ambao walikuwa wanamezea mate wadhifa wa Bw Odinga ni waliokuwa manaibu wa kiongozi wa chama Wycliffe Oparanya na Ali Hassan Joho, aliyekuwa mwenyekiti wa kitaifa John Mbadi na aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa katika ODM Opiyo Wandayi.

Kampeni hizo pia zilichangia chama hicho kuahirisha chaguzi za mashinani za ODM zilizoratibiwa kufanyika Aprili mwaka huu.

Sasa wanaofahamu yaliyotendeka waliambia Taifa Leo kuwa Bw Odinga aliamua kimakusudi kupendekeza wanne hao wateuliwe mawaziri ili kuzuia uwezekano wa kusambaratika kwa ODM.

“Baba aliruhusu maafisa wa zamani wa chama chetu kujiunga na baraza la mawaziri ili kuzima mvutano kuhusu urithi. Tayari kila mmoja wao alikuwa amechukua msimamo mgumu hali ambayo ilitishia uthabiti katika ODM,” akafichua afisa mmoja wa ODM kutoka Nyanza ambaye aliomba tulibane jina lake.

Mbunge mwingine pia aliunga mkono wazo hilo akisema; “Hawa watu hawakuwa tayari kukomesha kampeni. Walibuni kambi na kila mmoja alikuwa akisaka uungaji mkono kutoka kwa wanachama. Kila mmoja aliendelea kuelezea jinsi walivyokuwa bora zaidi kutwaa wadhifa wa kiongozi wa chama.”

Mkewe Bw Odinga alisemekana kumuunga mkono Bw Mbadi kwa wadhifa wa kiongozi wa ODM. Naye Bw Wandayi alipata uungwaji mkono kutoka kwa kakake Bw Odinga, Oburu Oginga. Bw Joho naye alishikilia kuwa yeye ndiye alifaaa kwa wadhifa huo sawa na Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa zamani wa Kakamega.

Lakini inasemakana Bw Odinga alipodokeza kuwa angewapendekeza kwa nyadhifa za uwaziri, wote wanne waliachana na azma yao ya kumrithi kiongozi huyo, hali iliyorejesha utulivu katika ODM.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino sasa anasisitiza kuhusu haja ya kufanyika kwa chaguzi za mashinani za ODM kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ikiwa lengo la kupendekeza viongozi wakuu kwa uteuzi kuwa mawaziri lilikuwa ni kuzima siasa za urithi ndani ya ODM, kwa hivyo huu ni wakati mwafaka kwa chama kuandaa uchaguzi wa mashinani,” akasema.“Chama cha ODM kinahitaji viongozi wapya watakaoleta ‘hewa nzuri’ katika uongozi wake,” Bw Owino anaongeza.