Habari za Kitaifa

ODM yamtaka Gachagua akomeshe sarakasi

Na RUSHDIE OUDIA September 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha ODM kimemtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua kukoma kulalamikia masuala ya kibinafsi na badala yake ajishughulishe na utoaji huduma kwa wananchi wote wala siyo eneo moja la nchi pekee.

Chama hicho kimemsuta Naibu Rais kwa kutumia muda mwingi kupiga kelele kuhusu tofauti zake za kibinafsi na Rais William Ruto, badala ya kushughulikia masuala muhimu ya kitaifa.

Wakiongea na wanahabari mjini Kisumu, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga na Katibu wa Masuala ya Kisiasa Rozah Buyu walisema taifa linakabiliwa na changamoto nyingi kama vile za kiuchumi, ukosefu wa ajira, wasiwasi katika sekta ya elimu na shida katika sekta ya afya.

Kulingana na maafisa hao wa ODM, Wakenya wanatarajia kwamba Rais na naibu wake watajitokeza kuhutubia umma katika runinga, watawaelezea namna na kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo vita dhidi ya ufisadi, usaidizi kwa wakulima na namna ya kuimarisha ugatuzi.

“Tunavunjwa moyo na kushangaa kwamba Naibu Rais alitumia muda wa saa mbili na nusu katika runinga ya kitaifa akiongea kuhusu namna aliondolewa kutoka jukwaa ya WhatsApp. Nina uhakika kuwa hayo siyo masuala yenye umuhimu kwa Wakenya. Hata kizazi cha Gen Z na kile cha X huzungumzia masuala muhimu wala siyo yale ya kuondolewa kutoka kundi la WhatsApp,” akasema Bi Wanga.

Viongozi hao walikuwa wakiongea saa chache baada ya Bw Gachagua kulaumu watu fulani ndani ya serikali ya Kenya Kwanza aliodai wanamhujumu na kumgonganisha na Rais William Ruto wakati wa mahojiano katika runinga ya Citizen Ijumaa, Septemba 20, 2024.

Wakati wa mahojiano hayo, Bw Gachagua alizungumzia njama ya kumwondoa afisini, ubabe wa kisiasa Mlima Kenya, mahusiano kati yake na bosi wake, Dkt Ruto, kutohudhuria shughuli za Rais, kutojuzwa kuhusu ratiba ya Rais, uhusiano kati yake na Uhuru Kenya na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.

Lakini ni hatua yake ya kuangazia masuala ya kibinafsi badala ya yale yanayoathiri Wakenya ndio yalionekana kuwakasirisha viongozi wa ODM.

“Awali Bw Gachagua alijitokeza na kuwaambia Wakenya kwamba ni “wenye hisa” pekee watakaonufaika katika serikali ya Kenya Kwanza. Lakini sasa imetukia kuwa watu wengine wameingia serikalini, inavyopasa, na sasa ameanza kutetemeka,” akasema Bi Wanga.