Habari Mseto

Mwanaharakati kortini akitaka kibali Wakristo waoe wake wengi ‘ili talaka zipungue’

Na EVANS JAOLA September 24th, 2024 2 min read

MWANAHARAKATI mjini Kitale amewasilisha kesi katika Mahakama Kuu akitaka Wakristo waruhusiwe kuoa wake wengi.

Kesi ya Bonface Koimburi Ndura inatazamiwa kuzua mdahalo mkali miongoni mwa Wakristo nchini na duniani itakapoanza kusikilizwa.

Bw Ndura anataka kuwepo ndoa za Kikristo za mke zaidi ya mmoja.

Anapinga sheria ya ndoa iliyotiwa saini na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2014.

Mwanaharakati huyo, ambaye pia mtaalamu wa mazingira, anapinga sheria hiyo akisema inanyima haki wanaume, hususan Wakristo, walio katika ndoa kuoa wake wengi.

Kesi hiyo, iliyowasilishwa kupitia wakili Dennis Wanyama, iko mbele ya Jaji Anthony Mrima na inatarajiwa kuibua mijadala kuhusu uhuru wa dini ya Kikristo, haki za kikatiba, na tafsiri ya sheria ya ndoa nchini.

Bw Ndura 78, ambaye pia ni mwandishi wa kitabu “Waliooa wake wengi pia wataenda mbinguni,” anadai mfumo wa sasa wa kisheria unaruhusu Wakristo kuoa mke mmoja pekee, unakiuka uhuru wa kidini kwa wale wanaotafsiri Biblia kwa kuamini katika ndoa ya wake wengi.

“Kanuzi ya Adhabu na Sheria ya Ndoa zinaweka vikwazo vya ndoa kwa Wakristo, huku dini zingine kama vile Kislamu zikiruhusu waumini wao kuwa na wake wengi,” alihoji.

Bw Ndura, ambaye alimuoa Anne Nduta kwa harusi katika Kanisa Katoliki la Thigio mnamo Februari 10, 1973 katika Kaunti ya Kiambu, anahisi kwamba amenyimwa fursa ya kuoa wanawake ambao amezaa nao watoto na anawasaidia.

Kulingana na mlalamishi, masharti haya hayakiuki tu Kifungu 32 cha Katiba ya Kenya – ambacho kinalinda uhuru wa dini na imani – lakini pia yanakiuka Kifungu 45 ambacho kinatoa haki ya kuoa na kuanzisha familia kwa misingi ya imani ya mtu binafsi.

Bw Ndura anataja watu katika Biblia kama vile Ibrahimu, Yakubu na Mfalme Suleimani ambao walikuwa na wake wengi, kama ushahidi kwamba ndoa ya wake wengi ina mizizi ya kihistoria na kiteolojia katika Ukristo.

“Sheria ya kisasa ya ndoa ya mke mmoja ni ya kikoloni ambayo inapingana na mafundisho ya jadi ya Kikristo,” anasema.

Vile vile, anadai marufuku ya ndoa ya wake wengi imechangia ongezeko la talaka nchini Kenya na idadi kubwa ya wanawake na wanaume wanaolea watoto kivyao bila kuwepo baba au mama mzazi.

Anasema ndoa ya wake wengi ni suluhu kwa changamoto hizi za kijamii, akitetea kile anachoita ni “muundo thabiti kabisa wa familia” katika jamii.

Mfanyabiashara huyo anataka vifungu vya sheria anavyopinga kutangazwa kuwa kinyume na katiba, na hivyo Wakristo kuruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja kihalali.

“Hatua hii italeta usawa wa kisheria kati ya jamii za Kikristo na Kiislamu ambako ndoa ya wake wengi tayari inatambuliwa. Wanaume wengi wa Kikristo walio na mke mmoja huwa na wapenzi wa kando kisiri lakini hawawezi kuwafichua kwa kuhofia athari za kisheria,” akahoji.