Habari Mseto

Lenku naye ajiunga na wanaomezea mate kiti cha Waiguru katika CoG

Na STANLEY NGOTHO September 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Kajiado Bw Joseph Ole Lenku ametangaza azma yake ya kumrithi Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kama Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG).

Baraza hilo limepanga kufanya Mkutano Mkuu Oktoba 6 ili kuchagua viongozi wapya baada ya muhula wa miaka miwili wa viongozi wanaohudumu kukamilika.

Gavana Waiguru alichaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza Mwenyekiti wa CoG 2022 pamoja na Bw Ahmed Abdullahi wa Wajir kama Naibu wake, na Stephen Sang wa Nandi kama kiranja.

Wakati huo, Gavana Lenku na Waiguru walionyesha nia ya kuongoza COG, lakini Bi Waiguru aliteuliwa bila kupigiwa kura baada ya mazungumzo yaliyopelekea Lenku kujiondoa.

Bw Lenku alithibitisha kuwa tayari aliwasilisha ombi lake kutaka kumrithi Bi Waiguru.“Ndio. Ninatangaza tena nia yangu ya kuwa Mwenyekiti wa COG kwa mara ya pili. Muhula wa viongozi wanaohudumu umekamilika. Timu mpya inakuja,” alisema Bw Lenku.

Hata hivyo, Gavana huyo hakutoa maelezo mengi kuhusu azma yake, lakini alifichua kuwa atatafuta uungwaji mkono kutoka kwa wenzake mkutanoni.

“Katika Baraza, viongozi wetu huteuliwa kwa mashauriano. Tunaangalia wagombea mbalimbali na tunachagua kwa makubaliano. Makubaliano hayo huamuliwa na ushawishi wa kuendeleza ajenda za COG,” alifafanua.

Gavana huyo atakabiliana na Bw Ahmed Abdullahi wa Wajir na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ambao tayari wanamezea mate kiti hicho.