Habari za Kitaifa

Mzozo wa Rais, naibu wake wahofiwa kupumbaza nchi huku raia wakihangaika

Na JUSTUS OCHIENG’ September 25th, 2024 2 min read

UHASAMA unaotokota kati ya Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua unatishia kugubika changamoto kadhaa nzito zinazolikumba taifa hili na kuchangia kupuuzwa kwa masuala muhimu ya kitaifa.

Sekta ya elimu, mojawapo ya zile muhimu nchini, inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wengine wa vyuo vikuu vya umma.

Aidha, kuna mjadala wa kitaifa unaendelea kuhusu ufisadi kufuatia kufichuliwa kwa mpango tata wa ukodishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Mvutano huo ulisababisha wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini kufanya mgomo hali ilivuruga shughuli katika uwanja wa JKIA na viwanja vingine vyenye shughuli nyingi nchini.

Taifa pia inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yenye uwezo wa kutekeleza majukumu yake kikatiba, kwani haina mwenyekiti na makamishna.

Kwa hivyo, haiwezi kuendesha chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Banissa, Magarini na Ugunja yasiyo na wabunge sawa na wadi tisa zisizo na wawakilishi.

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umetaja mivutano kati ya viongozi wakuu serikalini kama njama ya kukwepa kushughulikia masuala muhimu ya kitaifa.

Mnamo Jumatatu, chama cha Wiper kinachoongozwa na kinara wa Azimio Kalonzo Musyoka, kile cha Jubilee kinachoongozwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kile cha DAP-Kenya chake Eugene Wamalwa viliomba kushirikishwa katika kesi ya kupinga mpango wa ukodishaji wa uwanja wa JKIA kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Aidha, malalamishi yameibuliwa kwamba kampuni ya Apeiro Ltd, inayomiliki hisa nyingi zaidi katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, ilishinda zabuni ya kuweka mfumo wa kiteknolojia wa kufanikisha mpango wa Afya kwa Wote (UHC). Kampuni hii inayo uhusiano wa kibiashara na kampuni ya Adani Group.

Mvutano kati ya Rais Ruto na naibu wake Bw Gachagua umezidishwa na ripoti kuhusu njama ya kuwasilishwa kwa hoja ya kumtimua afisini Naibu Rais.

Isitoshe, baadhi ya viongozi ndani ya muungano tawala wa Kenya Kwanza wameanza kumezea mate kiti hicho kwa matumaini kuwa hoja hiyo itapitishwa.

Tayari Seneta wa Tana River Danson Mungatana ambaye ni mwanachama wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais Ruto, amewasilisha hoja ya kumlaani Bw Gachagua katika bunge la seneti.

Hatua hii inaashiria kuwa wandani wa Rais na Naibu wake wanatarajiwa kupambana vikali.

Hata kabla ya hoja ya kumtimua Gachagua kuwasilishwa majina ya viongozi wanane yametajwa kama wale wanapigiwa upatu kujaza nafasi hiyo.

Wao ni pamoja na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri na Waziri wa Utalii Rebecca Miano.