Jamvi La Siasa

Vigeugeu: Waliilani serikali, ila sasa watetezi sugu

Na CHARLES WASONGA September 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

VIONGOZI wa ODM walioteuliwa mawaziri sasa wamepiga abautani na kuwa watetezi wa sera za Serikali ya Kenya Kwanza ambazo walipinga hapo awali.

Katika siku chache zilizopita, mawaziri John Mbadi (Fedha), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), Opiyo Wandayi (Kawi) na Ali Hassan Joho wamewashangaza Wakenya kwa kuunga mkono yale ambayo wao wenyewe waliwaambia Wakenya kuwa sio mazuri na wanapasa kuyakataa.

Siku chache baada ya kuingia afisini mnamo Agosti 8, Waziri Mbadi alibadilisha msimamo kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024 uliokataliwa.

Bw Mbadi, ambaye mnamo Juni alipinga mapendekezo yote kwenye mswada huo, aliahidi kurejesha baadhi ya mapendekezo aliyodai yalikuwa “mazuri”.

Aliahidi kufanya hivyo kwa kupendekeza marekebisho kwenye sheria mbalimbali za ushuru.

“Ukweli ni kwamba, sio yote kwenye Mswada wa Fedha yalikuwa mabaya na yenye athari hasi kwa wananchi. Kulikuwa na vifungu vizuri ambavyo sasa tutavileta pamoja na kuona jinsi ya kuvirejesha bungeni, sio kama Mswada wa Fedha bali kama mapendekezo ya marekebisho ya sheria zilizopo za ushuru,” Bw Mbadi akasema mnamo Agosti 18 kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini.

Waziri alitoa mfano wa ushuru wa mazingira (eco-levy) wa asilimia 10 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, lakini zenye vitu vya kuchafua mazingira.

Isitoshe, wiki hii, Bw Mbadi ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa ODM, alionekana kuutetea mpango tata wa kukodishwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Akiongea Jumatatu alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uchukuzi, waziri alisema makubaliano kati ya kampuni hiyo na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) hayakuwa “yenye nia mbaya.”

“Kwa mfano, kulingana na stakabadhi za makubaliano hayo, Adani haitawafuta kazi wafanyakazi wa JKIA. Wasiwasi ambao wafanyakazi hao walikuwa nao, na kuchangia wao kugoma, sasa haufai kuwepo tena,” Bw Mbadi aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kiambu Karongo Wa Thang’wa.

Kamati hiyo inaendesha uchunguzi kuhusu suala hilo baada ya Seneta wa Kisii Richard Onyonka kudai kuwepo kwa njama fiche katika mchakato huo wa ukodishaji JKIA.

Kwa upande wa Bw Oparanya, sasa anaisifia Hazina ya Hasla akiitaja kama mojawapo ya njia za kupambana na umasikini.

“Hazina hii ni nzuri kwa sababu inatoa mikopo midogo kwa Wakenya wenye mapato ya chini ili waweze kujiinua kimaisha. Hii ndio maana sasa ninaiunga mkono kwa sababu ninaielewa. Lakini hapo zamani nilikuwa nikiipinga kwa sababu sikuifahamu vizuri,” Bw Oparanya akasema Agosti 23 alipofungua kongamano la wafanyabiashara wadogo (SMSEs) jijini Nairobi.

Aliahidi kuwa wizara yake itawaandama wale waliochukua mkopo huo na hawajalipa jumla ya Sh19 bilioni kufikia Septemba 9, mwaka huu.

Kabla ya uteuzi wake, waziri huyo ambaye alikuwa naibu kiongozi wa ODM, hakuchelea kuwahimiza Wakenya wachukue mkopo huo na wasiulipe.

“Hizi pesa za ‘Hustler Fund’ ni zenu kama wananchi, chukueni na msirudishe,” akasema mnamo Mei 4, mwaka katika mkutano wa hadhara Nairobi.

Naye waziri Wandayi ameonekana kujivuta kuwachukulia hatua wakuu wa kampuni ya kusambaza umeme nchini (KPLC) kutokana na ongezeko la visa vya kupotea ghafla kwa stima kote nchini.

“Nguvu za umeme zilipotea kote nchini isipokuwa maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa na Magharibi mwa Kenya kutokana na hitilafu kwenye mitambo ya kusafirisha kawi hii katika eneo la Loyangalani. Wahandisi wa KPLC wanajizatiti kurekebisha mitambo hiyo,” Bw Wandayi akasema mnamo Septemba 6.

Lakini tukio sawa na hilo lilipotokea Novemba 18, 2023, Bw Wandayi, wakati huo akiwa kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa alitaka wakuu wa KPLC wapigwe kalamu.

Kwa upande wake, Bw Joho ameapa kufanya kazi na Rais Ruto ambaye awali aliapa kutoshirikiana naye kwa njia yoyote ile.

“Ni washenzi pekee ambao huwa hawabadili misimamo yao. Kwa sababu mimi sio mshenzi nimebadili msimamo wangu na sasa niko tayari kuwahudumia raia kama waziri chini ya serikali yake. Kimsingi, sote kama viongozi walioko serikali na wale wa upinzani, huwahudumia Wakenya,” akasema Agosti 3, alipokuwa akihojiwa kubaini ufaafu wake kwa wadhifa wa Waziri wa Uchumbaji Madini na Uchumi wa Majini.