• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
SHAMBULIO: Tukio ni la kwanza kubwa tangu la chuo cha Garissa

SHAMBULIO: Tukio ni la kwanza kubwa tangu la chuo cha Garissa

Na VALENTINE OBARA

KENYA haijashuhudia mashambulio makubwa ya kigaidi tangu lile la mwaka wa 2015 katika Chuo Kikuu cha Garissa ambapo watu zaidi ya watu 150 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Kufikia jana wakati uvamizi ulipotokea katika Hoteli ya Dusit, Nairobi, mashambulio mengi madogo ya kigaidi yamekuwa yakitokea katika maeneo ya mpakani wa Kenya na Somalia.

Kwenye hotuba yake ya kufungua mwaka wa 2019, Rais Uhuru Kenyatta alikiri kwamba licha ya utulivu ambao umekuwa ukishuhudiwa kwa muda mrefu, magaidi bado hulenga kushambulia taifa hili.

Kulingana naye, mipango ya ugaidi imekuwa ikivurugwa nchini kutokana na ushirikiano wa raia na maafisa wa usalama ambao wamekuwa wakitia bidii zaidi kulinda nchi.

“Ninaomba kila Mkenya katika mwaka wa 2019 na baadaye azidi kukaa macho. Pigeni ripoti kwa maafisa wa serikali mkiona mtu mnayemshuku katika kijiji au mtaa wenu. Jueni wale waliowazunguka na msiruhusu magaidi wala wahalifu kujificha miongoni mwetu. Kila raia anahitajika kulinda taifa letu, jamii zetu na familia zetu,” akasema rais.

Mashambulio pia yamevurugwa kwa muda mrefu kwa sababu kumekuwepo na juhudi nyingi katika jamii kuhamasisha vijana dhidi ya kudanganywa kujiunga na makundi ya kigaidi, kwa mujibu wa hotuba hiyo ya rais iliyotolewa Desemba 31.

Mbali na kuzuiwa kutekeleza mashambulio ya kigaidi humu nchini, kundi la al-Shabaab limekuwa pia likizidi kuzimwa nchini Somalia kutokana na ushirikiano wa kikosi cha Wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AMISOM) na majeshi ya mataifa mengine kama vile Marekani.

Mwezi uliopita, serikali ya Amerika ilisema jeshi lake liliua magaidi 62 wa al-Shabaab kwa kutumia bomu lililorushwa kutoka angani. Ilisemekana Amerika pekee ilifanikiwa kuua magaidi wapatao 300 mwaka wa 2018.

Shambulio la jana lilitokea siki moja tu baada ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani, Nairobi, Bw Francis Andayi kuamua washukiwa watatu wa shambulio la Westgate lililotokea mwaka wa 2013 wana kesi ya kujibu.

Watatu hao ni Ahmed Abdi, Liban Omar na Hussein Mustafa. Mshukiwa wa nne wa shambulio hilo, Adan Dheg aliachiliwa huru kutokana na ukosefu wa ushahidi dhidi yake.

You can share this post!

Sababu ya Kenya kulengwa zaidi na magaidi kuliko mataifa...

SHAMBULIO: Ni miaka 3 kamili tangu Al Shabaab waue...

adminleo