Habari za Kitaifa

Kindiki: Nyeri, Nairobi ndio zinaongoza kwa watu waliotoweka wakati wa maandamano ya Gen Z

Na SAMWEL OWINO September 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAUNTI za Nairobi, Nyeri na Kirinyaga zinaongoza kwa idadi ya watu waliotoweka kufuatia maandamano dhidi ya serikali, kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya kamati ya bunge.

Takwimu zilizowasilishwa kwa kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu utawala na usalama wa ndani na Waziri Kithure Kindiki zinaonyesha kuwa, Nairobi ina watu 39 waliotoweka, Nyeri 29 na Kirinyaga 16.

Waziri alisema jumla ya watu 1,208 walikamatwa wakati wa maandamano dhidi ya serikali, watu 42 walikufa, miili miwili bado haijatambuliwa na 132 waliripotiwa kutoweka katika kipindi hicho.

Kulingana na waraka huo, Kaunti ya Nyandarua ina 13, Kitui tisa na Garissa watu wanane bado hawajapatikana.

Machakos ina watu sita waliopotea, Mombasa ina watu watano ambao bado hawajulikani waliko, Kaunti za Mandera na Kisumu zina watu wanne kila moja, Kajiado watatu huku Kaunti za Wajir na Tharaka Nithi zikiwa na mtu mmoja kila moja ambao walitoweka miezi miwili baada ya maandamano ya kupinga serikali.

“Ingawa hii ni idadi ya visa vya watu waliopotea vinavyoripotiwa kwa polisi, ni muhimu kutambua kwamba vinaweza kubadilika, hasa watu ambao walikuwa wameripotiwa kutoweka wakipatikana,” Prof Kindiki aliwaambia wabunge.

Uchanganuzi katika Kaunti ya Nairobi unaonyesha kuwa, eneo la katikati mwa jiji ndilo lina idadi kubwa zaidi ya waliotoweka wakiwa ni watu wanane, Ruai saba, eneobunge la Dagoretti sita, Kasarani watano, Kilimani wanne, Embakasi watatu na Kayole mtu mmoja bado hajapatikana.

Mwezi uliopita, Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi iliambia Kamati ya Utekelezaji na Uangalizi wa Katiba (CIOC) kwamba, takriban watu 50 waliuawa, 197 walijeruhiwa na 19 wakatekwa nyara wakati wa maandamano ya kupinga serikali.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) hata hivyo ilisema vifo vya watu wakati wa maandamano hayo ni 60 huku watu 66 wakitoweka.

Waziri alisema uchunguzi unaendelea na yeyote atakayepatikana na hatia ikiwa ni pamoja na maafisa wa polisi watachukuliwa hatua.