Jamvi La Siasa

Kilichompa Riggy G ujasiri wa kumlipua bosi wake wazi wazi

Na BENSON MATHEKA September 29th, 2024 3 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amepata ujasiri wa kupiga vita mipango ya kumtimua baada ya kuungwa mkono na Wazee wa Jamii za eneo la Mlima Kenya akazindua kauli mbiu ya kuwakabili wapinzani wake.

Huku akirushia mkubwa wake kiazi moto kwa kuapa kuwa iwapo wabunge watamuondoa mamlakani wanavyopanga, chama tawala cha United Democratic Alliance kitaporomoka ishara kwamba hatua yoyote ya kumng’oa itakuwa hasara kwa serikali.

Akiwa Kiambu Ijumaa wakati ambao wanaoongoza mpango wa kumuondoa mamlakani walisema hoja yao inaungwa na zaidi ya wabunge 300, Bw Gachagua alionekana kuchochea ngome yake ya Mlima Kenya kwa kuonya kuwa kuondolewa kwake mamlakani kutakuwa pigo kwa UDA na kuimarisha kauli mbiu yake ya “usiguse murima” anayotumia kuashiria kuwa masaibu yake yanatokana na msimamo wake wa kutetea maslahi ya wakazi wa eneo hilo na umoja wao.

“Kuzindua kauli mbiu ya ‘harambee- Usiguse Mlima’ ni mkakati wa kuonyesha wakazi kwamba wabunge wanaompiga vita hasa kutoka ngome yake kuwa hawatetei maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya,” asema Dkt Gichuki.

Bw Gachagua anashikilia kuwa ni rais pekee anayeweza kuidhinisha hoja ya kumtimua mamlakani na kauli zake zinaonyesha yuko tayari kupigana jino na ukucha kujinususuru bila kusaza yeyote akiwemo kiongozi wa chama cha UDA.

“Anachomaanisha Bw Gachagua ni kuwa ana hakika masaibu yake yanatoka kwa Rais Ruto na kwa kuwa wadhifa wake ni wa kuchaguliwa akiwa mgombea mwenza wa chama cha UDA, hawezi kubanduliwa peke yake, yeye na rais wanapaswa kuondolewa pamoja,” asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki na kuongeza kuwa hii ni kiazi moto cha kisiasa kwa Dkt Ruto ambaye alitegemea eneo la Mlima Kenya kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Anasema mbinu hii imewatia baridi baadhi ya wabunge kutoka eneo hilo waliokuwa wakimkosoa huku akiwadhihirishia wanaompiga vita kwamba wanatumiwa na wale wa kutoka maeneo mengine kuzua migawanyiko kwao nyumbani.

Hisia sawa zilitolewa na viongozi wa muungano wa jamii za eneo la Mlima Kenya – Gikuyu, Embu na Ameru waliosema ni watu binafsi wa Mlima Kenya wanaotumiwa kuzua migawanyiko.

“Kuna mtindo unaoibuka wa kugawanya jamii za GEMA unaojitokeza kupitia jaribio la baadhi ya watu wetu binafsi kugawanya jamii kuwa za Mashariki na Magharibi mwa Mlima Kenya,” alisema mwenyekiti wa Gema, Askofu Lawi Imathiu.

Duru zinasema kuwa Rais Ruto ambaye kimya chake kuhusu mpango huo kilichukuliwa kuwa anauunga mkono anawazia kubadilisha nia na huenda akauzima baada ya mkutano wa wabunge wa muungano tawala unaopangwa kabla ya hoja kuwasilishwa rasmi bungeni.

Duru hizo zinasema kumekuwa na juhudi za kichinichini za kuzima mipango ya kumtimua Gachagua huku wabunge wa maeneo tofauti wakikutana na kutathmini athari za hatua hiyo kwao na kwa nchi.

Mnamo Alhamisi, viongozi Gema walisema watasimama na Bw Gachagua huku wakisema Rais Ruto aliwahakikikishia kuwa sio sehemu ya hoja ya kumtimua naibu wake.

Lakini Bw Gachagua ameonya kuwa kuondolewa kwake kutaporomosha UDA na kuvuruga serikali akimtaka Rais Ruto kurejesha utulivu katika chama na serikali yake.

“Uliahidi kuwa hautaruhusu naibu wako kuteswa. Hata kama hautatimiza ahadi nyingine kwa sababu ya changamoto zizoepukika za kifedha, ahadi hii hahiitaji pesa, timizia watu wa mlima hii moja tu. Usiruhusu maafisa wako kuhangaisha naibu wako,” Bw Gachagua alisema katika mahojiano ya runinga siku kumi zilizopita.

Licha ya wanaompiga vita kumlaumu kwa kutoheshimu rais, Bw Gachagua anasisitiza kuwa ni kiongozi wa nchi pekee anayeweza kuagiza mchakato wa kumtimua uanzishwe na unaweza kufaulu tu ukiwa na baraka zake.

“Chama chetu cha UDA kina Rais na Naibu Rais, na tulipigiwa kura tukiwa pamoja. Kama haumtaki Gachagua, utamaliza UDA,” Bw Gachagua alisema kauli ambayo wachambuzi wa siasa wanasema ilielekzwa kwa Rais Ruto ambaye ameitisha mkutano wa wabunge wa muungano tawala wiki ijayo.

Wanaopanga kumtimua Gachagua pia wanapanga kuwasilisha hoja yao wiki ijayo na huenda wasifanye hivyo kabla ya kukutana na rais.