Wanaume wanavyokimbilia kunyolewa na kupokea masaji ya vinyozi wanawake
KATIKA miaka ya hivi karibuni kumeibuka vinyozi wa jinsia ya kike katika jumuiya ya biashara ambayo imetawaliwa na wanaume kwa muda mrefu.
Wanawake kuzamia biashara hii kumebadili mtazamo huku wamiliki wa vinyozi wakivuna wateja wengi zaidi pamoja na faida.
Vinyozi wanawake wanaonekana kuwa chaguo tofauti kwa sababu wanaleta mguso na mbinu mbadala katika sekta ya urembo.
Elizabeth Nyambura ni kinyozi ambaye hupiga kazi hii mjini Gatanga kaunti ya Murang’a.
Ni mmiliki wa kinyozi ambacho kimepata ufanisi sababu ya kuhusisha mbinu maalum katika tasnia ya urembo.
“Ninafurahia kuona wanaume wanavyochangamkia huduma zangu. Hali hii inanipa motisha sana kwa sababu ninajua wanachokitaka,” aliungama.
Masaji yavutia
Huku wateja wengi wa kiume wakimiminika dukani mwake, yeye hutoa huduma ya masaji kama chambo cha kuwavutia baada ya kuwanyoa.
Grace Ngaruiya, kinyozi mwingine wa kike kutoka mji wa Ruiru, amechangamkia mtindo sawia ya kuwarembesha wanaume.
Anasisitiza haja ya vinyozi wa kike kuwa na ustahimilivu na nidhamu ili kukabiliana na matatizo ya kufanya kazi na wateja wa kiume.
Hata hivyo, Ngaruiya amevuna wateja waaminifu, akibainisha kuwa wanaume wengi wanathamini umakini wa mguso wa unyoaji nywele unaotolewa na vinyozi wa kike.
Miriam Wambui, kinyozi mwingine wa kike stadi amejipatia umaarufu haraka katika uwanja huu baada ya kusomea taaluma ya urembo.
Akiwa na tajriba ya zaidi ya miaka miwili, Wambui amekuza shauku ya ustadi wake, akisema kuwa anafurahia kunyoa katika kiwango ambacho kinawaridhisha wateja wake.
Akiwa amejiimarisha katika sekta iliyotawaliwa na wanaume, Wambui anasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua hii kukabiliana nao ili aibuke kidedea.
Changamoto
Vinyozi hawa wa kike wanafichua baadhi ya changamoto zinazowakabili, wakisema kuwa baadhi ya wateja wa kiume wamekuwa wakitaka kutumia huduma hiyo kuwatongoza, wakati mwingine wakitarajia zaidi ya uhusiano wa kikazi.
“Wanaume wengine wanatumia nafasi hizi za kutangamana nasi ili watushawishi kuwa na uhusiano wa kimapenzi,” mmoja wao alikiri.
Licha ya biashara kuimarika, vinyozi wa kike pia wanakabiliwa na vikwazo vya kifedha.
Hii huwakumba aghalabu wanapotafuta bidhaa za urembo na kuzipata kwa bei ghali sababu ya kuongezwa kwa ushuru.
“Tunaomba sera za kibiashara zifanywe thabiti ili kuwatunza wanabiashara,” alieleza Wambui.
Mmoja wa wateja wa wanawake hawa wanasimulia jinsi wanavyofurahia huduma hizi.
“Huduma za wanawake ni bora zaidi na tunafurahia sana wanapotuhudumia,” alifunguka Zachary Gicheru.
Ushindani kwa wanaume
Baadhi ya vinyozi wa kiume walieleza hofu yao baada ya biashara hii ya kuingiwa na ushindani kutoka kwa wanabiashara wa jinsia ya kike.
Wanasema tukio hili limewaacha na faida ndogo au kutopata faida yoyote siku za hivi karibuni.
“Ili kukabiliana nao, imebidi tuwalete wanawake wa kufanya masaji katika vinyozi,” alikiri James Kanja, mwanabiashara mjini Ruiru.