Trump amdhalilisha Harris na kurejelea siasa zake za matusi
ALIYEKUWA Rais wa Amerika, Donald Trump, ameonekana kurejelea siasa zake za matusi na chuki baada ya kumrejelea mpinzani wake Kamala Harris kama mtu mwenye tatizo la kiakili ambaye anastahili kutimuliwa afisini na kushtakiwa kortini.
Harris ni Makamu wa Rais wa Amerika na alipewa tikiti ya kuwania urais kupitia Chama cha Democratic baada ya Rais Biden kujiondoa mnamo Julai 21.
Trump, ambaye alihudumu kama Rais wa Amerika kati ya 2016-2020, naye anawania kiti hicho kupitia Chama cha Republican.
Amekuwa akikosoa uongozi wa sasa kwa kurejesha taifa nyuma kutoka kwa hatua zilizopigwa kimaendeleo hapo awali.
Akihutubia halaiki ya wafuasi wake eneo la Erie, Pennsylvania, Trump alisema kuwa Harris alihusika na uvamizi wa raia wa Amerika kwenye mpaka wao na Mexico na akasema anastahili kutimuliwa afisini kutokana na sababu hiyo.
“Joe Biden alilemewa na ukongwe na akapoteza akili. Ni jambo la kusikitisha sana ila Kamala Harris, binafsi naamini alizaliwa akiwa na tatizo la kiakili,” akasema Trump.
“Kuna kitu kibaya na Harris, sijui ni nini lakini lazima kipo na mnajua. Kila mtu anafahamu hilo,” akaongeza kiongozi huyo wa Republican.
Ikiwa imesalia karibu mwezi mmoja pekee kwa uchaguzi kufanyika mnamo Novemba 5, Trump anaendelea kulenga maisha ya kibinafsi ya Harris japo baadhi ya wafuasi wa Republican wamekuwa wakiona heri amakinikie masuala atakayoyatekeleza kwa raia wa Amerika akichukua usukani.
Mara si moja Trump ametishia kuwashtaki wapinzani wake akiwemo Rais Biden na aliyekuwa mpinzani wake mnamo 2016, Hillary Clinton.
Harris hata hivyo hashughulishwi kuhusu Trump kulenga maisha yake ya kibinafsi. Alipoulizwa kuhusu hilo, hakutetereka akisema kuwa ni mbinu ambazo Trump amezoea kuzitumia dhidi ya wapinzani wake kwa kuwa hana mpango wa kuyashughulikia matatizo au changamoto za raia wa Amerika.
Trump mwenyewe anakabiliwa na kesi ya kughushi stakabadhi za kibiashara jijini New York na uamuzi unaomhukumu ulitolewa Mei. Anasubiri kufahamu adhabu ya kifungo atakachopewa mnamo Novemba 26 japo wengine wanadai ana kinga kisheria baada ya kuhudumu kama rais.
Anakabiliwa na kesi nyingine mbili kuhusu maandamano yaliyotokea baada ya kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa 2020 ambapo alibwagwa na Rais Biden. Jumapili alionekana kuashiria kuwa hajali iwapo atashindwa katika kura ya mwaka huu.
“Akishinda, halitakuwa jambo jema kwangu lakini sijali,” akasema kwenye mkutano huo wa kampeni.
Baadhi ya wandani wa Trump nao wamemtetea kuhusu kumvamia Harris ambaye ni mwanamke mweusi mwenye asili ya Asia Kusini. Wamesema sera za Harris hazina nguvu zozote za kulinda uhuru wa Amerika hasa kuhusu wahamiaji kutoka mataifa mengine.
“’Naamini Kamala Harris ni chaguo bovu kwa Amerika. Utawala wake huenda ukawa mbaya zaidi kuliko kile ambacho tumeshuhudia Biden akifanya akiwa mamlakani kwa miaka minne iliyopita,” akasema Seneta wa Republican na mwandani wa Trump, Lindsey Graham.