Msichana,17, ‘ajiteka nyara’ na mpenziwe kulaghai wazazi Sh6m
KATIKA kisa cha watoto kupotoka, msichana mwenye umri wa miaka 17 katika Kaunti ya Meru alidaiwa kupanga njama ya kujifanya ametekwa nyara kwa nia ya kuwalaghai wazazi wake Sh6 milioni.
Ingawa kilichomfanya kupanga kuwalaghai wazazi wake pesa hizo hakikufahamika mara moja, wapelelezi wanawahoji watu kadhaa na familia kwa lengo la kubaini kilichomsukuma kuchukua hatua hiyo.
Msichana huyo, pamoja na washirika wake, wamekamatwa na polisi.
Mwanafunzi huyo wa Kidato cha Tatu katika shule moja huko Imenti ya Kati alipatikana akipumzika katika nyumba ya mpenzi wake katika kijiji cha Kaing’inyo, Nthimbiri, takriban kilomita saba kutoka Meru Mjini.
Mwanafunzi huyo, pamoja na mpenzi wake na mvulana mwingine, ambaye pia ana umri wa miaka 17, walipanga utekaji nyara huo feki na kudai kwamba angeuawa iwapo fidia haingelipwa.
Afisa wa upelelezi wa jinai katika kaunti ya Meru, Samuel Bett alisema waliopanga njama walimpigia simu mama ya msichana huyo wakitumia nambari ya kibinafsi, na kuitisha pesa hizo kwa vitisho.
Msichana huyo aliondoka nyumbani kwao Igoji kutafuta kibali kutoka kwa shule moja huko Imenti ya Kati akisubiri kuhamishwa hadi shule moja jijini Nairobi.
Hata hivyo, aliungana na mpenzi wake ambaye anadai kuwa mfanyabiashara mtandaoni.
Mpenzi huyo alimwalika rafiki mwingine anayefanya kazi katika eneo la kuosha magari huko Kianjuri Imenti Kaskazini ambapo walipanga njama ya kusingizia ametekwa nyara kuwalaghai wazazi wake pesa.
Wavulana hao wawili ni wanafunzi katika shule ya upili iliyo karibu na Majengo huko Imenti Kaskazini.
Baada ya kushindwa kurejea nyumbani, mama ya msichana aliyefadhaika alipiga ripoti ya kutoweka kwa binti yake mnamo Septemba 24.
Baadaye, alianza kupokea simu za vitisho na habari kwamba binti yake alikuwa mikononi mwa watekaji nyara ambao wangemdhuru.
Katika mojawapo ya simu aliyopigiwa, mmoja wa vijana alimwambia kwamba simu ambayo ingefuata ingekuwa ya ‘kumjulisha mahali pa kuchukua mwili’.
Bw Bett alisema kuwa familia hiyo ambayo haikujua kuhusu njama hiyo, iliwasihi waliodai kuwa watekaji nyara wasimdhuru.
Alisema wapelelezi walianza kusaka ‘watekaji nyara’ tangu ripoti ya kutekwa nyara ilipotolewa, kabla ya kuvamia nyumba ya mpenzi wa msichana na kuwakamata watatu hao walipokuwa wametulia. Polisi walisema vijana hao walipatikana wakiwa na misokoto 20 ya bangi. Kulingana na polisi huenda, watatu hao wakashtakiwa kwa kula njama ya kulaghai, kuwa na mihadarati, miongoni mwa mashtaka mengine.
Mnamo Jumanne, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Nkubu, Rose Ongira aliruhusu polisi kuwazuilia watatu hao siku tano wakamilishe uchunguzi wao. Mahakama iliamuru washukiwa hao wazuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Igoji.