Makala

‘Wababaz’ walaumiwa kuchangia ongezeko la uavyaji mimba usio salama

Na FRIDAH OKACHI October 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA ya kijamii yamelaumu wanandoa wa kiume pamoja na viongozi wa kanisa kuchangia ongezeko la uanyaji wa mimba miongoni mwa wanawake na wasichana kwa kuwafadhili kutafuta huduma zisizo salama.

Mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake kutoka Shirika la Feminist Bi Editar Achieng, alisema idadi ya uavyaji usio salama inaongezeka kiholela kutokana na wafadhili maarufu kama ‘wababaz’ kutaka wasihusishwe kulea mtoto.

“Tunajua wale wanafadhili ni wanaume ambao wana wake zao, wengine ni viongozi wa kidini. Wanajificha na kupatia wasichana pesa ili waavye mimba. Wanakataa zile mimba kwenye umati wa watu lakini upande mwingine wanakuwa wepesi kutoa pesa za uavyaji,” alisikitika Bi Achieng.

Mataifa mengi Barani Afrika, uavyaji wa mimba unaruhusiwa kisheria ingawa chini ya hali zinazotofautiana na mara nyingi zenye vikwazo. Waathiriwa wakiogopa lawama za kijamii na kutafuta huduma kinyume na sheria.

Mtaa wa Kawangware, ulio na zaidi ya watu 300,000, Taifa Dijitali ilikutana na Silvia, 32, mama wa mtoto mmoja na ambaye ameavya mimba tano akihofia kulea katika mazingira yenye ufukara pamoja na kuogopa kufahamisha wazazi.

Silvia, alisema baada ya kukamilisha Kidato cha Nne, aliingia kwenye mahusiano na mwanamume ambaye alikuwa na familia nyingine. Mahusiano hayo yalipelekea kupata ujauzito aliolazimika kuavya kwa Sh3,000 pekee.

Wanaharakati kutoka mashirika mbalimbali wanaotetea haki za wasichana na wanawake. Picha|Fridah Okachi

“Alisema hataki mtoto nje ya ndoa na kunipa Sh3,000. Nilifika kwenye kituo afya cha binafsi, saa kumi na mbili asubuhi kabla ya wagonjwa wengi kuwasili. Yule mhudumu aliniwekea vyuma katika sehemu yangu ya siri. Haikuwa rahisi vile, uchungu ulikuwa mwingi lakini aliniruhusu kwenda nyumbani,” alisema Silvia.

Ujauzito wa pili Silvia alipendekezewa kuweka tembe mbili chini ya ulimi wake. Kulingana naye, usiku huo maumivu yalimzidia na kupelekwa katika kituo cha afya. Hali hiyo ikimpa wazo la kurejea mbinu ya kwanza kwenye ujauzito wa tatu hadi tano.

“Nilipofika hospitali, muuguzi aliniuliza iwapo nilijaribu kutoa mimba nikakana. Nikiwa kwenye foleni nilianza kutokwa na damu nyingi iliyosababisha kulazwa katika chumba cha wagonjwa kwa siku mbili,” alieleza Silvia.

Katika maadhimisho ya uavyaji mimba salama, Septemba 28, 2024, Mwanzilishi wa shirika la Vuguvugu la wanawake (Women Collective Kenya) Bi Ruth Mumbi, alilaumu watunga sera nchini kwa kuzuia wanawake na wasichana kupata haki ya uavyaji mimba kwa njia salama.

Bi Mumbi, alisema baadhi ya vikwazo kwenye sheria ya Kenya, vinawapa mianya wasichana wadogo kutafuta uavyaji usio salama ikipelekea maisha yao kuwa hatarini.

 “Visa ambavyo tunapata ni vingi mno na vya kuhuzunisha. Mwaka jana msichana wa miaka 17 alipata ujauzito, akaavya na kufa. Jamii yake ilikataa kujihusisha na mazishi yake hadi wakati mashirika ya kijamii yalijitokeza kugharamikia. Familia yake iliogopa kupatwa na unyanyapaa. Si muhimu kutenga mwanamke kutokana na uamuzi alioufanya,” alisema Bi Mumbi.

Alitaja kuwa, baadhi ya sera zilizotungwa nchini zimesababisha uavyaji mimba kuwa wa tabaka la wenye pesa na kisomo.

“Wanaofariki kutokana na kuavya mimba kwa njia isiyo salama ni wanawake wanaoishi kwenye mazingira duni kama Kawangware, Korogocho na Kibra. Hawajui kuna njia sahihi za kuavya, siasa zimefanya uavyaji wa mimba kuwa wa matajiri,” alifafanua Mumbi.