Makala

Arsenal wasikitisha mashabiki wa Man United kwa kuzima Southampton

Na GEOFFREY ANENE October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAOMBI ya mashabiki wa Manchester United kuona Arsenal wakiteleza yalikosa kujibiwa baada ya Bukayo Saka kuchangia asisti mbili na goli wanabunduki hao wakinyamazisha Southampton 3-1 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Emirates mnamo Jumamosi, Oktoba 5, 2024.

Vijana wa kocha Mikel Arteta walijipata goli moja chini baada ya Cameron Archer kumwaga kipa David Raya dakika ya 55 kabla ya Gunners kujibu kwa mabao kutoka kwa Kai Havertz (58), Martinelli (68) na Saka (88) na kulemea Saints kwa mara ya kwanza katika mechi nne.

Havertz alinufaika na shuti la Saka kuja miguuni mwake baada kuramba mlingoti.

Martinelli aliyejaza nafasi ya Raheem Sterling dakika ya 60, alipokea krosi safi kutoka kwa Saka na kuikamilisha kwa ustadi kwa kumwaga kipa Aaron Ramsdale karibu na mlingoti.

Nguvu-mpya Leondro Trossard, ambaye pia aliingia nafasi ya Gabriel Jesus dakika ya 60, alichangia katika kuzalishwa kwa bao la tatu baada ya mpira kutoka kwake kukosa kuondoshwa vyema na beki Yukinari Sugawara kabla ya Saka kuuweka nyavuni inavyostahili kwa mshambulizi.

Ushindi huo wa 400 wa Arsenal nyumbani ligini unadumisha rekodi nzuri wakiwa nyumbani dhidi ya Saints hadi mechi 25 (ushindi 17 na sare nane).

Liverpool watamba

Mechi za raundi ya saba zilianza na Liverpool kudumisha uongozi wao kwa kulima Crystal Palace 1-0 kupitia bao la Diogo Jota ugani Selhurst Park.

Kufuatia ushindi huo, Arne Slot sasa ni kocha wa kwanza wa Liverpool kushinda mechi tisa kati ya 10 za kwanza.

Nao Liverpool wamefanya hivyo sasa kwa mara ya tatu baada ya 1961-1962 na 1990-1991. Palace nao wamekamilisha michuano saba ya kwanza ya ligi bila ushindi, hii ikiwa ni mara yao ya tano baada ya 1992-1993, 1994-1995, 2004-2005 na 2017-2018.

Manchester City washinda 

Kyle Walker naye alifikisha mechi 400 kwenye EPL baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba Manchester City wakilemea Fulham 3-2 kupitia mabao ya Mateo Kovacic (mawili) na Jeremy Doku.

Fulham walitangulia kuona lango la City kupitia kwa Andreas Pereira dakika ya 26 na Rodrigo Muniz (88) ugani Etihad kabla ya mabingwa hao watetezi kuwanyamazisha.

Liverpool, City na Arsenal wanasalia katika nafasi tatu za kwanza kwa alama 18, 17 na 17, mtawalia.

Brentford almaarufu Bees, waliendeleza mtindo wa kufunga bao katika dakika ya kwanza wakiongeza masaibu ya Wolves kwa kuwapiga mishale 5-3 baada ya kupata mabao kutoka kwa Nathan Collins, Bryan Mbeumo (penalti), Christian Norgaard, Ethan Pinnock na Fabio Carvalho. Matheus Cuhna, Jorgen Larsen na Rayn Ait-Nouri walifunga mabao ya Wolves wanaovuta mkia.

Wenyeji West Ham walizoa ushindi wao wa kwanza kwa kupepeta Ipswich Town 4-1. Michail Antonio, Mohammed Kudus, Jarrod Bowen na Lucas Paqueta walitetemesha nyavu za Ipswich iliyojiliwaza na goli kutoka kwa Liam Delap.

Leicester waliwazaba Bournemouth 1-0 kupitia bao la Facundo Buonanotte ugani King Power. Ligi itaelekea mapumziko ya karibu majuma mawili baada ya mechi za Jumapili.

Matokeo na ratiba ya mechi za EPL

Oktoba 5 – Crystal Palace 0-1 Liverpool (2.30pm), Arsenal 3-1 Southampton (5.00pm), Brentford 5-3 Wolves (5.00pm), Manchester City 3-2 Fulham (5.00pm), West Ham 4-1 Ipswich (5.00pm), Leicester 1-0 Bournemouth (5.00pm), Everton vs Newcastle (7.30pm).

Oktoba 6 – Aston Villa vs Manchester United (4.00pm), Chelsea vs Nottingham Forest (4.00pm), Brighton vs Tottenham (6.30pm).