Dimba

Farasi ni watatu EPL Liverpool, Man City na Arsenal wakifukuzana, Man U wakiishiwa pumzi

Na MASHIRIKA October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

LONDON, UINGEREZA

MBIO za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zimechacha mapema msimu huu mpya 2024-25 huku timu vigogo Liverpool, Manchester City na Arsenal zikifukuzana kwa karibu baada ya mechi saba pekee tangu msimu uanze Agosti.

Liverpool wako kileleni kwa pointi 18, wakifuatwa na Man City walio na alama 17 sawa na Arsenal baada ya mechi za wikendi.

Diogo Jota alifungia vinara hao bao la pekee na la ushindi dhidi ya Crystal Palace katika uga wa Selhurst Park mnamo Jumamosi kuwezesha kikosi hicho cha kocha Arne Slot kusalia kileleni mwa jedwali hilo lenye timu 20.

Mabingwa watetezi Man-City walitoka nyuma kushinda wageni Fulham 3-2 katika uwanja wa Etihad siku hiyo hiyo ya Jumamosi. Kiungo mkabaji Mateo Kovacic alitinga goli dakika ya 32 kusawazisha baada ya Andreas Pereira kuweka wageni kifua mbele dakika ya 26.

Kovacic kisha akaongeza la pili dakika ya 47 lililofanya Man-City kupiku Fulham huku winga Jeremy Doku akiongeza la tatu dakika ya 82 kuongeza mwanya wa ushindi.

Hata hivyo, Rodrigo Muniz alifungia Fulham bao la pili dakika ya 88 na kuwapa mashabiki wao tumaini finyu la uwezekano wa kuondoka angalau na pointi moja iwapo wangelifunga lingine la tatu, lakini dua yao haikufua dafu kwani Man-City walikaa ngangari kuzoa alama zote tatu katika ushindi huo wa 3-2.

Katika uwanja wa Emirates, wenyeji Arsenal waligutushwa na bao la Cameron Archer dakika ya 55 lililoweka Southampton kifua mbele.

Wangu wangu straika Kai Havertz akafanya mambo 1-1 dakika ya 58 kufungua ukurasa wa mabao kabla Gabriel Martineli (68′) na Bukayo Saka (88′) kuhakikisha wenyeji wanashangilia ushindi wa 3-1 na mashabiki wao nyumbani.