Habari Mseto

Wasomi wa Kiislamu wafufua mjadala wa miraa, wataka marufuku ya kilimo hicho

Na CECIL ODONGO October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASOMI wa dini ya Kiislamu wametoa wito kwa serikali ikome kuvumisha na kufadhili kilimo cha miraa, wakisema mmea huo hauna manufaa yoyote kwa uchumi na una athari hasi katika jamii.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Viongozi wa Kiislamu (NAMLEF), Abdullahi Abdi, aliwaongoza wasomi hao kuweka marufuku dhidi ya mauzo ya miraa. Bw Abdi alisema miraa imeharibu maisha ya watu binafsi, familia zao na jamii nzima kwa hivyo, watapigana sana iondolewe.

“Tunaomba serikali ibadilishe sheria au kurekebisha sheria ambazo zinaunga kilimo na biashara ya miraa na ikome kufadhili kilimo hicho. Inastahili kufanya hivi kwa kuwazia afya na maslahi ya kijamii badala ya manufaa ya kiuchumi,” akasema Bw Abdi.

Alikuwa akiongea katika Msikiti wa Jamia baada ya kuwaongoza zaidi ya wasomi 500 kutoka jamii ya Kisomali Kaskazini mwa Kenya kuzungumzia athari za miraa miongoni mwa vijana.

“Hatutaruhusu mauzo ya miraa katika maeneo yetu ndiposa tunatoa wito kwa serikali kusaka njia nyingine ya watu wanaotegemea kilimo cha miraa kupata riziki.”

“Pia tutahakikisha kuwa wale ambao wana uraibu wa miraa wanapelekwa katika kituo cha urekebishaji wa tabia. Kama wasomi, tunaapa kuwa tutakikisha serikali inawajibikia hili,” akaongeza Bw Abdi.

Wasomi hao waliahidi kufanya kazi na kaunti za Kaskazini Mashariki mwa Kenya na Waislamu wote kuhakikisha kuwa zao la miraa ni marufuku katika eneo hilo.

Marufuku hiyo ya miraa inakuja baada ya kaunti sita za Pwani mnamo Juni mwaka huu kupiga marufuku muguka ambayo ni aina ya miraa. Kaunti hizo ni Mombasa, Lamu, Kwale, Kilifi, Tana River na Taita Taveta.

Wakati huo magavana wa kaunti hizo walisema kuwa wengi wa wagonjwa waliokuwa na matatizo ya kiakili walipatikana wakiwa na uraibu wa kutumia muguka. Pia walilalamika kuwa matumizi ya muguka ambayo ni bei rahisi na ni rahisi kuvuna, yalikuwa juu sana miongoni mwa vijana.

Hata hivyo, viongozi wa Kaunti za Embu na Meru ambako muguka hukuzwa sana walipinga marufuku hiyo wakisema kuwa hiyo ilikuwa njama ya kuwavuruga kibiashara.

Mnamo Jumapili, Bw Abdi alisema kuwa safari ya kushirikiana na misikiti, viongozi wa kijamii, makundi ya vijana na makundi ya kijamii imeanza na watahakikisha miraa ni marufuku kaunti za Kaskazini mwa Kenya.

“Serikali haistahili kuweka mbele faida badala ya maslahi ya raia. Hawafai kupuuza matatizo ya kiafya na kiakili ambayo yanasababishwa na miraa,” akasema Abdi.