Habari za Kitaifa

Si leo, ni wiki ijayo: Maseneta wapitisha kusikiza kesi ya kutimuliwa kwa Gachagua Oktoba 16-17

Na MARY WANGARI October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SPIKA wa Seneti Amason Kingi ameagiza kikao cha Seneti kusikiza hoja ya kumtimua Naibu Rais wiki ijayo, Jumatano na Alhamisi.

Hii ni baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kukosa kuunga mkono pendekezo la Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot la kubuniwa kwa Kamati Maalum ya maseneta 11 kusikiza hoja ya kumtimua Gachagua.

Seneti sasa itakuwa na muda wa siku mbili kusikiza mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais.

Maseneta Samson Cherargei (Nandi) Enoch Wambua wamehoji kuwa muda huo hautoshi. Spika Kingi amesema Seneti itahakikisha kila upande umepata muda wa kutosha kujitetea na kuwasilisha upande wake.

“Hakutakuwa na malalamishi yoyote baada ya shughuli hii. Ikiwa Jumatano na Alhamisi hazitoshi tuna Ijumaa
Tutaongeza muda kulingana na masuala yanavyojitokeza.”

Kingi anewaonya maseneta dhidi ya kuzungumzia kwa kutoa matamshi/maandishi kuhusu mienendo ya Naibu Rais au mchakato wa ufurushaji kwa jumla nje ya kikao cha Seneti.