Gachagua akosa nyota tena kortini
NAIBU Rais Rigathi Gachagua, Jumanne alishindwa tena jaribio la 26 la kutaka kuzima mchakato unaoendelea wa kumuondoa madarakani lilipokataliwa na korti.
Mahakama Kuu jijini Nairobi ilikataa ombi la Bw Gachagua la kuzuia seneti kutojadili mchakato wa kumng’atua mamlakani kuanzia leo.
Kesi 26 zimewasilishwa kortini tangu bunge la kitaifa lilipoanza ukusanyaji wa saini kuunga hoja ya kumtimua mamlakani lakini hakuna jaji aliyetoa agizo la kumpendelea Bw Gachagua.
Kesi hizo zimewasilishwa na Bw Gachagua mwenyewe au kupitia washirika wake.
Jumanne, katika uamuzi kuhusu kesi ya hivi punde, Jaji Chacha Mwita alisema kwamba Bunge linapaswa kuruhusiwa kutumia mamlaka yake.
Jaji huyo alisema mahakama zinafaa kusita kuchukua majukumu ya asasi zingine za serikali kumaanisha alikataa ombi la kuingilia shughuli za seneti kusikiliza na kujadili mashtaka 11 katika hoja ya kumtimua Gachagua iliyopitishwa na Bunge la Kitaifa.
Jaji, hata hivyo, alisema ombi la Bw Gachagua linaibua maswali makubwa ya sheria na kuagiza faili hiyo ipelekwe kwa Jaji Mkuu Martha Koome, ili ateue jopo la majaji kusikiliza na kuamua kesi hiyo.
Jaji Mwita aliendelea kusema kuwa Jaji Mkuu anaweza kuagiza kesi hiyo isikizwe na jopo ambalo tayari limeteuliwa kuamua kesi zingine sita.
“Baada ya kuzingatia maombi, hoja na mawasilisho kutoka kwa pande zote na kuangalia katiba na sheria, ombi la kutoa amri ya muda ( kuzuia seneti kujadili hoja ya kumtimua Gachagua) limekataliwa,” alisema jaji.
Bw Gachagua aliwasilisha kesi mpya Ijumaa iliyopita, akitaka kuzuia Seneti kushughulikia hoja ya Bunge la Kitaifa kuidhinisha kuondolewa kwake kama Naibu Rais.
Bw Gachagua alikuwa amelalamika kuwa hakupatiwa muda wa kutosha kusikilizwa kwa haki na kanuni za ushirikishaji wa umma hazikutimizwa.
Kupitia kwa wakili Paul Muite, Bw Gachagua alisema alilazimika kuwasilisha kesi hiyo mpya kufuatia matukio mapya, ikiwemo anayodai kuwa ya ushirikishaji duni wa umma ambao uliendeshwa na Bunge la Kitaifa.
Alisema ushirikishaji wa wananchi uliendeshwa katika ngazi za kaunti na Mahakama Kuu ikaamuru ufanyike katika maeneo bunge.
Hata hivyo, Bw Gachagua alisema ilani haikutosha na ndiyo sababu watu wachache- 224,000 walishiriki katika shughuli hiyo kote nchini.
Anatoa mfano wa zoezi hilo katika eneo bunge la Keiyo Kusini akieleza kuwa takwimu haziwiani kwani ni watu 43 pekee waliojitokeza kwa zoezi hilo na inadaiwa 70 kati yao waliunga mkono kuondolewa kwake ofisini huku watatu wakipinga.
Bunge la Kitaifa lilipinga ombi hilo na kumshutumu Bw Gachagua kwa kusema kesi hiyo ilikuwa ikiibua masuala sawa na yaliyowasilishwa katika kesi zingine ambazo zinasubiri kusikizwa na majaji watatu.
Mahakama pia iliarifiwa kwamba uamuzi wa kuidhinisha hoja ya kumuondoa Gachagua mamlakani ulifuata sheria na katiba na kwamba alisikizwa kwa kufuata katiba alipofika mbele ya Bunge la Kitaifa na kujitetea.
Seneti kwa upande wake ilisema kuwa mahakama hazifai kuingilia mchakato wa kikatiba uliowekewa muda wa kukamilika.
Zaidi ya hayo, Seneti ilisema mahakama inapaswa kusubiri mchakato huo ukamilike kuendeshwa kulingana na katiba na sheria na kisha kuhoji uadilifu wake ikiombwa kufanya hivyo.
Jaji aliambiwa Bw Gachagua ana fursa ya kufika mbele ya Seneti na kutoa ushahidi wake.