Sababu ya korti kupiga breki sherehe ya Kindiki na kumpa matumaini Gachagua
PROFESA Kithure Kindiki aliyeteuliwa kuwa Naibu Rais wa tatu wa Kenya huenda akasubiri hadi Alhamisi ijayo kuapishwa baada ya Mahakama Kuu kusimamisha kujazwa kwa nafasi iliyoachwa baada ya kutimuliwa kwa Bw Rigathi Gachagua.
Mchakato wa kumuidhinisha Profesa Kindiki ulikuwa umeharakishwa katika Bunge la Kitaifa kabla ya Bw Gachagua kupata maagizo mawili kutoka Mahakama Kuu kusitisha kujazwa kwa wadhifa wa naibu rais.
Katika agizo la kwanza, Jaji Chacha Mwita alisimamisha kujazwa kwa wadhifa huo hadi Oktoba 24 kesi ya Bw Gachagua itaposikilizwa na jopo la majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Vile vile, Jaji Richard Mwongo wa Mahakama Kuu ya Kerugoya alitoa agizo sawa katika kesi iliyowasilishwa na washirika wa Gachagua hadi Jaji Mkuu ateue jopo la majaji kuisikiliza Oktoba 24.
Agizo hilo lilitolewa saa chache baada ya Wabunge 236 kuidhinisha uteuzi wa Profesa Kindiki kujaza nafasi ya Bw Gachagua ambaye amelazwa hospitalini na kuchapishwa kwa uamuzi wa wabunge hao na Spika Moses Wetang’ula kupitia toleo spesheli la gazeti rasmi la serikali.
Agizo hilo lilijiri ikibaki hatua moja tu ya waziri huyo wa usalama wa ndani kuapishwa kuwa naibu rais.
Katika kesi hiyo, Bw Gachagua alitaja mchakato wa kumtimua Bungeni na kuondolewa madarakani kuwa kejeli kwa Katiba, akisema Wabunge walitegemea madai ya uwongo ili kumzima kisiasa.
Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alimshutumu Rais Ruto kwa kuhusika katika mchakato wa kumtimua.
Alisema mfadhili wa mchakato wa kumuondoa mamlakani, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, mashahidi aliowaita, na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) hawakuthibitisha mashtaka yoyote dhidi yake.
Wakili wa Gachagua, Paul Muite anasema katika kesi hiyo kuwa, Seneti ilitumiwa katika njama ya kumtimua afisini.
Wakili huyo mkuu alisema licha ya Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi na Maseneta kufahamu kuwa Gachagua alikuwa mgonjwa na kukimbizwa katika hospitali ya Karen, walikataa ombi la kumruhusu kupata matibabu kabla ya kuwasilisha ushahidi wake.
Kulingana na Muite, hakukuwa na haja ya kuharakisha shughuli za Seneti, kwa vile hakuna ratiba iliyowekwa ili kikao hicho kikamilishwe na kuamua hoja.
Maseneta waliidhinisha mashtaka matano na kutupilia mbali sita ambayo Mutuse alishtaki Gachagua katika hoja yake.
Hata hivyo, Gachagua anasisitiza kuwa, alihukumiwa bila kusikilizwa kwani alikuwa na ushahidi wa kukanusha madai hayo.
“Mlalamishi aliugua wakati wa kusikilizwa kwa hoja hiyo Oktoba 17, 2024 kutokana na hali hiyo, alikimbizwa hospitalini na kulazwa kwa matibabu ya dharura. Katika hali ya kushangaza, Seneti ilipiga kura ya kuendelea kusikiliza mashtaka na kumnyima haki yake ya kusikilizwa kwa haki. Haki zake chini ya Kifungu cha 50(1) cha Katiba zilikiukwa,” anahoji Bw Muite.
Kulingana na wakili huyo mkuu, Kingi alikiuka katiba kwa kuruhusu ushahidi mpya ambao haukuwasilishwa mbele ya Bunge la Kitaifa kukubaliwa.
Alidai kuwa haki ya mwanasiasa huyo ilishinda ya Seneti kuharakisha kumtimua.
Kulingana na Muite, Bunge la Kitaifa tayari lilikuwa limetangaza Ijumaa kuwa kikao maalum cha kumshughulikia mteule huyo.
Hata hivyo, aliteta kuwa Bunge haliwezi kumuidhinisha mrithi wa Gachagua bila Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC) kuwa na makamishna.
Kwa sasa, Prof Kindiki anahudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, jukumu ambalo ameshikilia tangu Oktoba 2022, akapumzishwa kati ya Julai 11, 2024 na Agosti 8, 2024, wakati Rais alivunja Baraza lake la Mawaziri.
Mafanikio ya Kindiki
Akiwa Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Taifa, Prof Kindiki ameongoza na kusimamia mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na: Mpango wa Uboreshaji wa Vifaa vya Polisi kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa huduma za usalama za Kenya; kukamilika kwa mfumo mkakati wa kuanza utekelezaji wa kuboresha Polisi yaliyopendekezwa na jopo lililoongozwa na Jaji mstaafu David Maraga na kuimarisha vita dhidi ya ujangili na ukosefu wa usalama kwa ujumla kote nchini miongoni mwa mafanikio mengine.
Kabla ya kuteuliwa Waziri na Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki alihudumu kama Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi, kuanzia 2013, ambapo pia alihudumu kama Naibu Spika wa Seneti; pamoja na Kiongozi wa Wengi katika Seneti.
Akiwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti, aliongoza ajenda ya kutunga sheria ya chama cha wengi katika Seneti.
Kindiki pia amefundisha sheria na kushikilia nyadhifa mbalimbali za utawala katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Moi na kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alianza taaluma yake kama Mhadhiri Msaidizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Moi punde tu baada ya kuhitimu na shahada ya kwanza ya sheria.
Kisha alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama Mhadhiri baada ya kuhitimu Shahada ya Uzamifu katika Sheria ya Kimataifa ambapo alipandishwa cheo haraka hadi Mkuu wa Idara ya Sheria ya Umma akiwa na umri wa miaka 33 na kisha kuwa Msimamizi Msaidizi akiwa na umri wa miaka 35.
Baadaye Kindiki alipandishwa cheo kuwa Profesa Mwandamizi wa Sheria.
Ameandika machapisho thelathini na matano yakiwemo vitabu, sura za vitabu na makala katika majarida nchini na kimataifa.
Profesa Kindiki ana Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Diploma ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M), na Shahada ya Uzamifu (Ph.D.) katika sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini.
Aliwakilisha Rais Ruto katika kesi iliyomkabili katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.